1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

England wapata ushindi mwembamba dhidi ya Austria

7 Julai 2022

England wameanza kampeni yao ya kuwania ubingwa wa Ulaya kwa wanawake kwa kupata ushindi mwembamba wa bao moja kwa bila dhidi ya Austria mbele ya mashabiki 69,000 uwanjani Old Trafford usiku wa kuamkia Alhamis.

https://p.dw.com/p/4DmKB
Frauen EM England - Österreich
Picha: Martin Rickett/PA/AP Photo/picture alliance

Wenyeji hao katika dakika za awali za mechi walionekana kuzidiwa maarifa na wageni wao ila walimakinika baadae na katika dakika ya 16 ya mechi Fran Kirby alimtolea pasi nzuri Beth Mead na mshambuliaji huyo anayeichezea klabu ya Arsenal akatumia ujuzi wake kwa kuupitisha mpira juu ya mlinda lango wa Austria ambaye ni mwenzake katika klabu ya Arsenal, Manuela Zinsberger, na kuwaweka England uongozini katika kile kilichogeuka na kuwa goli la pekee la mechi hiyo iliyokuwa na burudani tele.

Timu hizi zilipopatana mara ya mwisho kwenye mechi ya kuwania kufuzu kwenye Kombe la Dunia mwezi Novemba, England walipata ushindi wa moja bila pia kwani Austria waliwapa ushindani mkali na nusra wasawazishe katika mechi hiyo.

England kupata kibarua kigumu zaidi katika mechi yao ya pili

England sasa watakutana na Norway katika mechi yao ya pili siku ya Jumatatu huko Brighton katika kile kinachoonekana kwamba kitakuwa kibarua kigumu zaidi kwao katika awamu ya makundi. Norway wanatarajiwa kuwapa kitisho kikubwa England katika kundi A kwa kuwa mchezaji wao bora ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji bora duniani Ada Hegerberg kurudi kwenye timu ya taifa baada ya kuamua kutocheza kandanda la kimataifa kwa miaka mitano.

England - Österreich
Mlinda lango wa Austria Zinsberger akiokoa shuti la Lauren Hemp wa EnglandPicha: Oli Scarff/AFP

Austria nao watakuwa wanacheza na Ireland Kaskazini ambao wanashiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa hiyo hiyo Jumatatu, mechi hiyo ikichezwa Southampton.

Alhamis mechi itakuwa moja pia ya kundi A ambapo Norway watakuwa wanachuana na hao Ireland Kaskazini mwendo wa saa tatu usiku saa za Ulaya ya kati.

Ijumaa mechi zitakuwa mbili ambapo katika kundi B Ujerumani watakuwa wanapambana na Denmark kisha Finland watakuwa na kibarua watakapopatana na Uhispania.

Tukiwazungumzia hao Uhispania ni kwamba azma yao ya kuuchukua ubingwa wa Ulaya imepata pigo baada ya mchezaji wao nyota ambaye ndiye mchezaji bora duniani kwa sasa Alexia Putellas kupata jeraha la goti hapo juzi Jumanne wakati wa mazoezi.

Jeraha hilo la Putellas si pigo tu kwa Uhispania bali kinyang'anyiro kizima cha Euro kwa kuwa mchezaji huyo wa kiungo cha kati anayeichezea Barcelona alikuwa anatarajiwa awe mmoja wa nyota wa mashindano haya. Uhispania ilikuwa ndiyo timu inayopigiwa upatu na wengi kunyakua ubingwa wa mwaka huu, shukran kwa klabu ya Barcelona kutawala kandanda la wanawake Ulaya.

Lakini sasa Putellas ndiye mchezaji wa pili muhimu kwa Uhispania kuondolewa kikosini baada ya mfungaji magoli bora Jennifer Hermoso kupata jeraha la goti pia wiki kadhaa zilizopita.

Uhispania wako "kundi la kifo"

Ikikumbukwe kwamba Uhispania wako katika kundi gumu linaloitwa "kundi la kifo" ambalo linajumuisha Ujerumani ambao wamelishinda taji hili mara nane, Denmark ambao walifuzu fainali mwaka 2017 na Finland.

Frankreich Paris | Ballon d'Or | Siegerin Alexia Putellas
Kiungo wa Barcelona na Uhispania Alexia Putellas akipokea tuzo ya mchezaji bora duniani Ballon d'Or ya mwaka 2021Picha: Henri Szwarc/Xinhua/IMAGO

Mechi nyengine inayotarajiwa kuleta msisimko katika duru ya makundi ni mpambano wa kundi C kati ya Uholanzi ambao ndio mabingwa watetezi watakapokwaana na Sweden. Kundi D nalo linajumuisha Ufaransa, Ubelgiji, Italia na Iceland. 

Zaidi ya tiketi nusu milioni zimeuzwa kwa mashabiki katika nchi 100 kote duniani. Mechi ya Jumatano ambayo ndiyo iliyokuwa ya ufunguzi kati ya England na Austria ilishuhudia tiketi zote kuuzwa na mashabiki kuujaza uwanja nayo fainali itakayochezwa katika uwanja wa Wembley mnamo Julai 31, tiketi zake zote nazo zimekwisha uzwa.

Mashindano haya ya Euro 2022 yalikuwa yanastahili kuchezwa mwaka 2021 ila yakasogezwa mbele kwa kuwa mashindano ya wanaume yalicheleweshwa kwa mwaka mmoja kutokana na janga la virusi vya corona.