1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yatiwa moyo na uchaguzi

31 Oktoba 2010

Katika uchaguzi huu, Umoja wa Ulaya umesambaza waangalizi sehemu nyingi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na waangalizi hao wanaona kwamba kwa jumla uendeshaji wa uchaguzi ulikuwa wa kuridhisha.

https://p.dw.com/p/Pv41
Sehemu ya kundi la waangalizi 42 wa Umoja wa Ulaya kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania 2010
Sehemu ya kundi la waangalizi 42 wa Umoja wa Ulaya kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania 2010Picha: EUEOM

David Martin ni mkuu wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya, EU, katika uchaguzi huu wa nne chini ya mfumo wa vyama vingi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Umoja wake, ni miongoni mwa wafadhili wakubwa wa shughuli za kimaendeleo nchini Tanzania, likiwemo hili suala la uchaguzi.

Martin anasema kwamba, kwa ujumla hali ya amani ilitawala vituo vya upigaji kura vilipofunguliwa, ingawa kulikuwa na mapungufu ya hapa na pale, likiwemo suala la ukosefu wa vifaa vya kupigia kura katika baadhi ya maeneo na au wapiga kura kuwasili vituoni bila ya kukuta majina yao kwenye orodha za wapiga kura.

"Miongoni mwa matatizo tuliyoyagundua ni yale ya watu kuwasili vituoni wakiwa hawajui wanatakiwa kupiga kura chumba kipi, lakini kwa ujumla tunashawishika kwamba hadi kufikia jioni ya leo, kila aliyetaka kupiga kura atakuwa ameweza kupiga kura yake." Amsema Martin.

Kampeni zilivyokuwa kuelekea uchaguzi wa leo (31 Oktoba 2010)
Kampeni zilivyokuwa kuelekea uchaguzi wa leo (31 Oktoba 2010)Picha: DW

Ukilinganisha taswira ya kujitokeza wapiga kura katika uchaguzi wa mara hii, Martin anasema kwamba safari hii huenda idadi ikawa ni ndogo inapolinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2005.

Hadi sasa ni matukio machache tu yaliyoripotiwa kupitia vyanzo mbali mbali, ambayo yanaweza kuashiria kuwepo kwa hali zisizo za kawaida katika uchaguzi huu. Hata visiwani Zanzibar, ambako kawaida nyakati kama hizi, huwepo na ripoti nyingi za uharibifu wa uchaguzi na au uvunjaji wa haki za binaadamu, mara hii hali imetulia.

Kisiwani Pemba, ambako ndiko kwenye ngome ya upinzani ya Chama cha Wananchi (CUF), watu walijitokeza na mapema asubuhi kupiga kura zao katika hali ya amani. Mgombea ubunge wa jimbo la Mkanyageni kwa tiketi ya CUF, Mohammed Habib Mnyaa, aliiambia Deutsche Welle mapema leo hii (31 Oktoba 2010) kwamba, watu wengi wamejitokeza kupiga kura zao.

"Kinachoonekana ni misururu mirefu ya wanawake na wanaume, wanapiga kura kwa salama usalimini. Mpaka saa hizi hali kisiwani Pemba ni shwari, na mimi sijapata taarifa zozote ikiwa kuna eneo lenye matatizo." Alisema Mnyaa.

Hata hivyo, kutokana na mazoea ya kutokuendeshwa chaguzi huru na za wazi visiwani Zanzibar, lolote ambalo lilitia shaka, liliweza kupandisha hisia kali miongoni mwa wapiga kura, kama anavyosema Martin kuhusu hali ya wasiwasi kidogo uliozuka asubuhi hii Zanzibar.

"Hakujakuwa na matatizo makubwa Zanzibar, lakini kulikuwa na hali ambapo vifaa vya kupigia kura havikuwasili kwa wakati katika vituo vinne vya uchaguzi, na hilo likazua mtafaruku wa kiasi fulani." Amesema Martin.

Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia kwenye uchaguzi wa vyama vingi na matokeo ya safari hii, yanatarajiwa kupatikana mapema zaidi kuliko hapo awali. Tume zote mbili za uchaguzi, ile ya Taifa, NEC, na ile ya Zanzibar, ZEC, zilisema kwamba, zimejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa safari hii, matokeo yanapatikana haraka iwezekanavyo.

Mwandishi: Mohammed Khelef

Mhariri: Othman Miraji