EU yaahidi kuisaidia Tanzania kuwahudumia wakimbizi | Matukio ya Afrika | DW | 29.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

EU yaahidi kuisaidia Tanzania kuwahudumia wakimbizi

Mabalozi wa EU wametoa ahadi ya kuendelea kutoa misaada ya kiutu kwa wakimbizi wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC walioko Tanzania.

Wakati wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya wakifikia mwafaka kuhusu mzozo wa wakimbizi kwa kuanzisha kituo cha kuwapokea na kuwahudumia waomba hifadhi kwenye mataifa ya Afrika, nchini Tanzania mabalozi wa umoja huo wametoa ahadi ya kuendelea kutoa misaada ya kiutu kwa wakimbizi wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC.

Hayo yamebainishwa na mabalozi 11 kutoka Umoja wa ulaya wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania ambao wanazuru mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kukagua shughuli za kuhudumia wakimbizi katika kambi ya Nduta inayohifadhi wakimbizi kutoka Burundi.

Akiongea katika mkutano wa pamoja na wakuu wa mashirika yanayotoa huduma kwa wakimbizi, balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Roeland Van de Geer, amebainisha kuwa jamii ya kimataifa inatambua changamoto za wakimbizi kwa nchi inayowapokea wakimbizi na kwa wakimbizi wenyewe

Wakati huo huo, Serikali ya Ujerumani imetenga kiasi cha Euro milioni 3 sawa na shilingi bilioni 780 kwa ajili ya misaada kwa wakimbizi na wenyeji mkoani Kigoma

Akizungumza na DW katika ziara ya mabalozi wa Umoja wa Ulaya katika Kambi ya wakimbizi wa Burundi ya Nduta mkoani Kigoma, Balozi Detlef Waechter amesema nusu ya pesa hizo zitasaidia wakimbizi na nyingine ni kwa ajili ya maendeleo kwa wenyeji wa wakimbizi

Wakimbizi wa Burundi wakiwa wamebeba virago vyao kuabiri boti katika ziwa Tanganyika eneo la Kigoma

Wakimbizi wa Burundi wakiwa wamebeba virago vyao kuabiri boti katika ziwa Tanganyika eneo la Kigoma

Balozi huyo wa Ujerumani amesisitiza kuwa kutokana na uzoefu wa nchi yake katika kuhifadhi wakimbizi anautambua mzigo unaoikabili serikali ya Tanzania na kwamba kupitia katika mfuko wa pamoja wa Umoja wa Ulaya, Ujerumani itaendelea kutoa misaada kwa wakimbizi na maeneo yanayowahifadhi.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa idara ya wakimbizi nchini Tanzania, Harrison Mseke, amewaambia mabalozi wa Umoja wa Ulaya kuwa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa fedha kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi jambo linalozorotesha utoaji wa huduma kambini na usafirishaji wa warundi wanaohitaji kurejea nchini mwao.

Changamoto kubwa ambayo imetajwa na mkurugenzi huyo wa wakimbizi nchini Tanzania ni upungufu wa vyumba vya madarasa, huduma za nishati ya kupikia, nyumba na upungufu wa chakula.

Jumla ya mabalozi 11 wa nchi za Umoja wa Ulaya wamehitimisha ziara ya siku tatu mkoani Kigoma kukagua utekelezaji wa miradi ambayo nchi zao zinatoa fedha kusaidia wakimbizi na Watanzania.

Tanzania inahifadhi takribani wakimbizi 349,000 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na wengi wao wanaishi katika mkoa wa Kigoma, magharibi wa Tanzania.
 

Mwandishi: Prosper Kwigize/DW Kigoma

Mhariri: Mohammed Khelef