1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

EU itakuwa na ushiriki gani kiusalama nchini Mali, 2023?

3 Januari 2023

Huku ghasia zikiendelea mwaka huu mpya wa 2023 nchini Mali, wataalam wa usalama wanatoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuimarisha uwepo wao nchini humo licha ya changamoto zilizopo.

https://p.dw.com/p/4LfKG

Mizozo iliyoshuhudiwa na watawala wa kijeshi wa Mali na uhusiano wao wa karibu na mamluki wa Urusi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, vimesababisha nchi za Ufaransa, Ujerumani na washirika wao wa Umoja wa Ulaya kusitisha operesheni za kiusalama katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi mwaka huu, jambo linaloashiria hatari zaidi za kiusalama nchini humo.

Frankreich Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Dominique Jacovides/abaca/picture alliance

Mwezi Februari, Ufaransa ilitangaza kuwa vikosi vyake nchini Mali vitaondoka baada ya takriban miaka kumi ya mapigano katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ulianza kuzorota wakati utawala wa kijeshi wa Mali ulipochukua mamlaka katika mapinduzi ya mwaka 2021.

Soma zaidi: ECOWAS yaanza kutekeleza vikwazo vyake dhidi ya Mali

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema nchi yake haiwezi kuendeleza ushirikiano wa kijeshi na mamlaka ambazo hazina malengo na mikakati sawa. Macron aliongeza kuwa wanajeshi na misheni zinazoongozwa na Ufaransa zitatumwa mahali pengine katika eneo la Sahel.

Umoja wa Ulaya kujiondoa pia Mali

Straßburg | Josep Borell
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep BorellPicha: Jean-Francois Badias/AP/picture alliance

Miezi miwili baadaye, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell alitangaza kwamba ujumbe wa mafunzo ya kijeshi wa Umoja huo uitwao EUTM, utasitisha shughuli zake baada ya kubainika ushirikiano kati ya jeshi na mamluki wa Urusi kutoka Kundi la Wagner, lenye uhusiano wa karibu na Kremlin. Washirika wa Wagner wameshutumiwa kwa udhalilishaji mkubwa katika nchi za Syria, Ukraine na Mali.

Soma zaidi: Chanzo cha mzozo wa Mali na mshirika wake Ufaransa

Wakati huo huo, Ujerumani imetumia miezi kadhaa kujadili suala la uwepo wa wanajeshi wake nchini Mali. Vikosi vya Ujerumani vimeshiriki katika mipango miwili ya kijeshi nchini Mali, ambayo ni ujumbe wa mafunzo wa Umoja wa Ulaya na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kama MINUSMA.

Uhusiano wa Mali na kundi la Wagner

Lakini uhusiano wa karibu wa taifa hilo la Afrika na Kundi la Wagner ulisababisha serikali ya Ujerumani kukubaliana kuwa itaanza kuwaondoa wanajeshi wake katikati ya mwaka huu wa 2023 na kuwaondoa kabisa ifikapo Mei mwaka 2024. Tangazo hilo lilijiri baada ya Uingereza kutangaza kuwa itaondoa kikosi chake mapema zaidi ya tarehe iliyopangwa ya Desemba 2023.

Niederlande | Macky Sall | Präsident von Senegal und Leiter der Afrikanische Union
Rais wa Senegal na wa Umoja wa Afrika Macky SallPicha: JEROEN JUMELET/ANP/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop na Waziri wa Ulinzi Kanali Sadio Camara walipongeza mazungumzo ya pande mbili na washirika wa Ulaya wanaotaka ushirikiano katika kudumisha usalama nchini humo. Rais wa Umoja wa Afrika Macky Sall ametoa wito wa kuwepo mshikamano zaidi na mataifa ya Afrika katika ukanda wa Sahel.

Soma zaidi:Serikali ya Mali yazuia jaribio la mapinduzi 

Katika mahojiano na DW mwezi Februari, muda mfupi kabla ya Ufaransa kutangaza kuwaondoa wanajeshi wake, Sall alisema ikiwa hakuna amani na usalama barani Afrika, basi dunia haitakuwa na amani na usalama.

Hali ya usalama nchini Mali

Tangu mwaka 2012, hali ya usalama nchini Mali imekuwa ya sintofahamu, huku makundi kadhaa yanayotaka kujitenga yakipambana dhidi ya serikali na kuanzisha mapinduzi na vikosi vya itikadi kali na kuua watu wengi kaskazini na katikati mwa Mali.

Mali | Colonel Assimi Goita
Kanali Assimi Goita, Kiongozi wa kijeshi nchini MaliPicha: Malik Konate/AFP

Wakati kikosi cha kijeshi kinachoongozwa na Kanali Assimi Goita kikiendelea kusalia madarakani, hali ya usalama mashinani ni ya kutisha mno hasa kaskazini na katikati mwa Mali.

Serikali ya Mali imekuwa ikikanusha kushirikiana na mamluki wa Urusi kutoka Kundi la Wagner na Rais wa Urusi Vladimir Putin amewahi kusema kuwa Kremlin haina uhusiano wowote na mamluki hao katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Soma zaidi:Makundi ya kigaidi nchini Mali yashambulia kambi ya jeshi 

Kuondoka kwa vikosi vya kigeni kumeonyesha mustakabali usiyo wa wazi kuhusu amani na usalama nchini Mali mwaka ujao. Wakati baadhi ya raia wakishirikiana na mamlaka za ndani katika harakati za ulinzi wa taifa, watu wengine wamedhihirisha nia ya kutafuta njia mpya za kushirikiana na askari wa kigeni ili kukabiliana ipasavyo na ugaidi.