EU, AU wakubaliana kuimarisha ushirikiano | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

EU, AU wakubaliana kuimarisha ushirikiano

Umoja wa ulaya na Afrika wakubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja muhimu ikiwa ni pamoja na uhamiaji, usalama, uwekezaji katika elimu na maendeleo endelevu kwenye mkutano uliokamilika nchini Ivory Coast.

Suala la uhamiaji ni mojawapo ya masuala mazito yaliyojadiliwa kwa kina katika mkutano huo na kufikiwa maamuzi. Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk akizungumzia suala zima la uhamiaji ametaja juu ya biashara ya utumwa nchini Libya akiitaja ripoti hiyo kuwa ya kuogofya huku akitilia mkazo kwamba suala la uhamiaji ni jukumu la pamoja baina ya serikali za Ulaya na Afrika.

Wasafirishaji haramu wa binadamu wachemshiwa muarobaini

Katika mkutano huo mjini Abidjan, viongozi kwa pamoja wamekubaliana kuhusu mpango wa dharura wa kuyaangamiza makundi yanayofanya biashara ya binadamu na kuwarejesha nyumbani wahamiaji katika jitihada za kupunguza janga la ukiukaji haki za binadamu nchini Libya. Alpha Conde rais wa Guinea ambaye nchi yake ndiye mwenyekiti wa kupokezana wa Umoja wa Afrika ameweka wazi juu ya kile kilichofikiwa kuhusu wahamiaji.

Libyen Flüchtlinge in Sabratha (Reuters/H. Amara)

Baadhi ya wakimbizi waliyoko nchini Libya

“Tumechukua uamuzi juu ya kuwahamisha haraka  wakimbizi, na kuunda kamati inayoongozwa na tume  ya umoja wa afrika juu ya haki za binadamu, ikisaidiwa na umoja wa Ulaya, wanaowatafuta wafanyabiashara ya binadamu, na tunaona ukiukwaji huu kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, na hivyo, nchi mbalimbali lazima ziweke vikosi maalum vya kupambana  dhidi ya mtandao wa kusafirisha watu kwa njia za magendo.”

Makala ya televisheni yawafumbua watu macho

Picha zilizooneshwa hivi karibuni nana kituo cha Televisheni cha CNN mapema mwezi huu zilizoonyesha wahamiaji wakipigwa mnada kama watumwa na walanguzi wa binadamu  huko nchini Libya na hivyo kuibua hamaki barani  Ulaya na ghadhabu barani  Afrika.

Taarifa hiyo iliangazia juu ya ukiukwaji uliofanywa dhidi ya wahamiaji wa Afrika wanaotaka kuingia Ulaya, ikilazimisha suala hilo kuwa ajenda kuu ya mkutano huo ambao ulilenga kuzingatia maendeleo ya vijana wa Afrika.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema Jumatano kuwa mpango huo ulihusisha uanzishwaji wa "jopokazi" ikijumuisha polisi wa Ulaya na Afrika pamoja na maafisa wa kijaasusi.

Serikali ya Libya yawajibika

Elfenbeinküste EU-Afrika-Gipfel in Abidjan (Reuters/P. Wojazer)

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Mpango huo uliibuka kutoka mkutano wa viongozi wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa muungano wa ulaya  na wawakilishi wa serikali kutoka Chad, Niger, Morocco, Congo na Libya ambao uliitishwa na Ufaransa Jumatano.

Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa walikubaliana kuzuia  mali pamoja na kuweka vikwazo vya kifedha dhidi ya walanguzi wanaojulikana.

Serikali ya Libya, iliyoahidi kuchunguza  ripoti za mnada wa watumwa, ilikubali kuyaruhusu mashirika ya umoja wa mataifa kufikia kambi za wahamiaji katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake, viongozi wa Ujerumani walisema.

Nchi za Umoja wa ulaya, wakati huo huo, zimeridhia  kufadhili mpango wa kuwarudisha  wahamiaji kutoka Libya, mchakato ambao tayari unaandaliwa na shirika la kimataifa la uhamiaji,IOM.

Wahamiaji walio na matatizo ambao hatimaye wanaweza kuhifadhiwa watapelekwa  nchini chad au Niger kabla ya kuhamishwa kwenye nchi ya tatu inayoweza kuwa nchi ya  Ulaya au kanda nyingine.

Mwandishi: Fathiya Omar/RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu


 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com