1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yajitetea kuyafungia mashirika ya kiutu

Lilian Mtono
4 Agosti 2021

Ethiopia imetetea uamuzi wake wa kuyasimamisha kwa muda mashirika mawili ya misaada ya kiutu ambayo bado yanafanya shughuli zake kwenye jimbo la Tigray lililoharibiwa vibaya na vita.

https://p.dw.com/p/3yXfH
Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed
Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Mashirika hayo ya Madaktari wasio na mipaka, MSF tawi la Uholanzi na shirika la kuhudumia wakimbizi la Norway, NRC yamesimamishwa kwa miezi mitatu. Hatua hii ni pigo la karibuni kabisa kwenye mchakato wa utoaji wa misaada ya kiutu kwenye jimbo la Tigray linalokabiliwa na mzozo, na ambako Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya watu wanateseka na njaa.

Mashirika hayo mawili yalizungumzia kwa uwazi kuhusiana na kusimamishwa kwao jana Jumanne, yakisema yalikuwa yakitafuta taarifa zaidi kutoka kwa mamlaka.

Kwenye taarifa iliyochapishwa hii leo, Ethiopia imesema kwa pamoja mashirika hayo ya MSF na MCR yamekuwa yakisambaza taarifa za uwongo kwenye mitandao ya kijamii na kukiuka  malengo na mamlaka ambayo mashirika hayo yalipewa ili kufanya kazi kwenye eno hilo.

Soma Zaidi: Asilimia 90 ya raia wa Tigray wanahitaji msaada wa kiutu

Hata hivyo taarifa hiyo haikutoa mifano ya taarifa hizo za uongo.

Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ameonya kuhusu kuyazushia madai mashirika ya kiutuPicha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu madai dhidi ya watoa misaada ya kiutu.

Mkuu wa misaada ya kiutu kwenye Umoja wa Mataifa Martin Griffiths, hapo jana alionya kuhusiana na madai dhidi ya mashirika ya kiutu, na kutaka tuhuma dhidi yao kuachwa mara moja. Alisema wakati akihitimisha ziara yake ya siku sita nchini Ethiopia.

Amesema, "Madai mapana dhidi ya watoa misaada ya kiutu yanatakiwa kuachwa.Kwa nini, kwa sababu sio sawa. Hayana msingi wowote. Yanatakiwa kuendana na ushahidi, kama upo. Na kusema ukweli ni ya hatari."

Serikali ya Ethiopia pia inayatuhumu mashirika hayo kwa kuwaajiri watumishi wa kigeni ambao hawakuwa na kibali halali cha kufanya kazi na kusema MSF waliingiza vifaa vya satelaiti ya radio kinyemela.

Taarifa hiyo imeongeza kwamba shirika la tatu la Al Maktoum limesimamishwa kwa sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kushindwa kusimamia hatua za kujikinga na virusi vya corona na matumizi mabaya ya fedha. Shirika hilo la Dubai linajihusisha na masuala ya elimu, lakini haijajulikana kama nalo lilifanya kazi Tigray.

Mashirika hayo yamekuwa yakionya kuhusu hali mbaya Tigray.

Katibu mkuu wa shirika la wakimbizi la Norway, NRC Jan Egeland mara kadhaa ametumia ukurasa wake wa twitter kuonya kuhusuiana na hali tete ya kiutu katika jimbo la Tigray.

Mwezi Februari aliwahi kuandika na hapa nanukuu, "hakuna haja ya kufichaficha, misaada bado haiwafikii raia wenye mahitaji makubwa katika jimbo la Tigray.

Madaktari wasio na Mipaka, mwezi Machi lilielezea hali ya kutisha inayochochewa na machafuko ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela ya takriban watu wanne walioshushwa kwa nguvu kutoka kwenye basi la abiria na kuuliwa na wanajeshi.

Samanta Power an der Central American University in San Salvador
Samantha Power, mkuu wa misaada ya kiutu wa nchini Marekani amewataka wanamgambo wa TPLF kuondoka Tigray mara moja.Picha: Jose Cabezas/REUTERS

Katika hatua nyingine, mkuu wa misaada wa Marekani Samantha Power amevitolea mwito vikosi vya waasi vya TPLF kwenye jimbo la Tigray kuondoka mara moja kwenye mikoa ya Amhara na Afar inayopakana na Tigray wakati mzozo kwenye jimbo hilo ukitishia kusambaa kote nchini Ethiopia.

Soma Zaidi: Mzozo wa Tigray unaweza kuchochea vurugu za kikabila

Power amesema hayo kupitia ukurasa wa twitter jana jioni akiwa ziarani nchini Athiopia na kusema ili misaada iweze kuingia Tigray pande zote zinatakiwa kusitisha uhasama na kuongeza kuwa hakuna suluhu itakayopatikana kwa nguvu za kijeshi.

Mashirika: AFPE