1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia na Eritrea zaparuana

Sylvia Mwehozi22 Juni 2016

Maafisa wa Eritrea wamesema, Ethiopia inanuia kuanzisha vita kamili dhidi ya taifa hilo, wakati wakijitetea mbele ya Baraza la Umoja wa Mataifa juu ya tuhuma za makosa dhidi ya ubinadamu.

https://p.dw.com/p/1JBAU
Äthiopien Soldat an der Grenze zu Eritrea
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Wanajeshi wa nchi hizo mbili walianzisha mapambano katikati ya mwezi huu, wote wakitupiana lawama kwa kuanzisha uchokozi dhidi ya mwenzake.

Wiki iliyopita, waziri wa mambo ya nje wa Eritrea aliishutumu Marekani kwa kuhusika katika mgogoro huo akimaanisha "uchochezi wa taifa hilo" kwa shambulizi lililofanywa na vikosi vya Ethiopia. Eritrea yenyewe pia ilisema askari 200 wa jeshi la Ethiopia waliuawa.

"Tunapozungumza hivi sasa, Ethiopia inafanya maandalizi makubwa ya kijeshi na inanuia kuanzisha vita rasmi" amesema mshauri wa rais wa Eritrea Yemane Ghebreab wakati akizungumza mbele ya baraza la Umoja wa Mataifa.

Anaendelea kusema kwamba "Ethiopia inafikiria tuhuma nyingi dhidi ya Eritrea kama kisingizio, na kwamba inaweza kutokea sasa au isitokee kabisa. AInasema wale wanaoilaumu Eritrea hawawezi kuangalia upande mwingine na kuona uhalifu wa ubinadamu unaofanywa na Ethiopia kwa watu wake na kuanzisha vita."

Alipoulizwa nini kimefanya Eritrea kutoa onyo dhidi ya utayari wa kijeshi wa Ethiopia, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba, kumekuwa na kauli hizo kwa muda mrefu pamoja na kushuhudia kile kinachoendelea katika ardhi na kwamba kuna askari wengi sasa wanaopelekwa mpakani. Eritrea inasema ipo tayari kwa ajili ya kujilinda.

Mshauri huyo tayari ameandika malalamiko rasmi kwa baraza hilo kufuatia kuuawa kwa waeritrea 18 katika mapigano ya hivi karibuni.

Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi Eritrea
Watoto wakicheza katika kambi ya wakimbizi EritreaPicha: Reuters/T. Negeri

Ethiopia kwa upande wake inadai kwamba pande zote mbili ziliathirika na mapigano hayo licha ya kushindwa kutoa maelezo ya kina, inaamini kwamba hali haitakuwa mbaya.

Msemaji wa serikali ya Ethiopia Getachew Reda akizungumza mapema mwezi huu alisema kwamba vikosi vya jeshi la nchi hiyo vilichokozwa na vile vya Eritrea, akionya kuwa, "Ninaamini kwamba wakati huu, hawatafanya ujinga na kurudia makosa ya kutualika katika vita.Tumechagua kuepuka vita, na ndio maana tumeyaondoa majeshi yetu, mara tu malengo yetu yatakapofikiwa."

Umoja wa Mataifa umeushutumu utawala wa Eritrea kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo, mateso, ubakaji na mauaji kwa miaka 25 ukitaka kesi hiyo kupelekwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu .

Wanaishutumu pia nchi hiyo kwa kuwatia utumwani watu wapatao laki tatu hadi nne pamoja na kuendesha sera ya upigwaji risasi katika mipaka yake ili kuwazuia watu wasikimbilie nje ya nchi .

Eritrea imeyakana madai hayo yote, ikisema kwamba karibu watu laki mbili wametia saini ombi la kuiunga mkono serikali.

Wawakilishi wa Somalia, Djibouti na Kenya wameliambia baraza hilo kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kuja na mbinu mpya ya kulinda na kukuza haki za binadamu nchini Eritrea.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef