1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia kufanya duru ya uchaguzi wa pili bila ya Tigray

Sudi Mnette
21 Septemba 2021

Ethiopia imesema haitoendesha duru ya pili ya uchaguzi katika majimbo takribani 26 katika duru ijayo ya mchakato huo ya kitaifa kutokana na masuala ya kiuslama.

https://p.dw.com/p/40afs
Äthiopien | NEBE | Soliana Shimelis
Picha: Solomon Muchie/DW

Katika duru ya kwanza ya mwezi Juni, Chama cha Waziri Mkuu Abiy Ahmed, Prosperity Party kiliweza kushinda muhula wa miaka mitano kwa kudai kushinda viti vya ubunge 410 kati ya viti 436 vya bunge la shirikisho.

Lakini changamoto za usambazaji wa vifaa na ukosefu wa usalama vilisababisha ucheleweshaji wa kufanyika kwa zoezi hilo katika maeneo mengine, kwa hivyo duru ya pili ya uchaguzi imepangwa kufanyika Septemba 30.

Msemaji wa bodi ya uchaguzi, Solyana Shimeles amesema katika uchaguzi huu wa sasa, zaidi ya wapiga kura milioni 7 watawachagua wawakilishi 47 wa bunge la shirikisho, na viti vingine 105 vya uwakilishi wa majimbo. Hata hivyo ameongeza kusema fursa hiyo haitapatikana kwa majimbo 18 ya eneo la Amhara na manane ya Oromia. "Bado hatujaamua kwa jinsi gani na lini uchaguzi utafanyika katika maeneo haya. Hata hivyo, kwa vile idadi ya majimbo ni ndogo, tutaamua lini ambapo tutafanya uchaguzi kwa pamoja katika maeneo yote hayo," alisema Solyana.

Vita na machafuko ni kikwazo cha kudumu katika jimbo la Tigray

Äthiopien Mekele | Pro-TPLF Rebellen
Wapiganai wa kundi la TPLF mjini MakelePicha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Eneo la Amhara limekuwa na madoa ya mapigano kati ya majeshi ya serikali na kundi la wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF, wakati Oromia inapambana na uasi wa Jeshi la Ukombozi la Oromo OLA.

Uchaguzi huo pia hautafanyika katika baadhi ya majimbo ya kama ya Afar na Benishangul-Gumuz, bodi hiyo ilisema, ingawa haikutoa ufafanuzi wa idadi ya maeneo lengwa. Kwa ujumla Ethiopia ina majimbo 547, lakini bodi ya uchaguzi haikurodhesha Tigray, ambayo kwa sehemu kubwa kwa sasa ipo katika udhibiti wa TPLF.

Serikali mpya ya taifa hilo imepangwa kuundwa Oktoba 4. Lakini msemaji wa bodi ya uchaguzi Solyana amesema matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa Septemba 30 yatatangazwa Oktoba 10.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliingia madarakani mwaka 2018 kwa kuungwa mkono na maandamano kadhaa ya kuipinga serikali iliyokuwepo kwa wakati huo na hivyo kutoa ahadi ya kuvunja historia ya kimabavu ya Ethiopia kwa  kiasi fulani kufanya chaguzi za kidemokrasia ambazo haizajawahi kufanyika nchini humo.

Chanzo: AFP