1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia: Amnesty yadai 'mauaji ya wengi' yamefanyika Tigray

John Juma
13 Novemba 2020

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema watu wengi waliuawa katika jimbo lenye machafuko la Tigray Ethiopia, katika kile wanachokiita kuwa ‘mauaji ya halaiki‘.

https://p.dw.com/p/3lEzs
Äthiopien Gondar | Amhara Miliz
Picha: Eduardo Soteras/AFP

Walioshuhudia mauaji hayo wamevilaumu vikosi vya usalama vinavyounga mkono chama tawala katika jimbo hilo katika vita vyake dhidi ya serikali kuu. 

Kwenye ripoti yake, shirika la Amnesty International limesema limethibitisha kuwa takriban mamia ya watu walijeruhiwa au waliuawa kwa kukatwa katika mji wa Mai-Kadra kusini magharibi mwa jimbo la Tigray, usiku wa Novemba tisa.

Hicho kilikuwa kisa cha kwanza kuripotiwa cha mauaji ya raia wengi kufuatia machafuko ya wiki moja kati ya chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray ‘Tigray People's Liberation Front‘ (TPLF) na serikali ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, aliyeshinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka uliopita.

Ripoti ya Amnesty International imejiri siku sawa na ambayo vikosi vya ABiy Ahmed vilifaulu kudhibiti maeneo mengi ya magharibi mwa Tigray, huku maelfu ya Waethiopia wakiendelea kukimbia kuelekea Sudan, na hivyo kusababisha wasiwasi wa kuzuka kwa janga la kibinadamu. Abiy alivipongeza vikosi vyake kwa kukomboa maeneo ya magharibi mwa jimbo hilo akisema ni ushindi  kwa wanajeshi waliokabiliana na mashambulizi mabaya na mauaji ya kikatili.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Minasse Wondimu Hailu/picture alliance/AA

Viokosi vya Ethiopia vyakomboa magharibi mwa Tigray

Abiy ameongeza kuwa "ni ushindi kwa raia wasiokuwa na hatia wa Mai-Kadra ambao walikuwa wakiuawa kinyama na chama cha TPLF wiki hii. Na kwa Watigray wanaopenda amani na wafanyao bidii katika majukumu yao, lakini ambao wametengwa na Waethiopia wenzao kufuatia, chuki woga na propaganda ta TPLF”

Kando na hayo katika mji mkuu Addis Ababa, serikali ya Ethiopia imeanzisha kampeni y akuchanga damu ili kuwasaidia walioathiriwa kufuatia mgogoro huo wa Tigray. 

Mamia ya watu wamejitokeza kutoa damu katika uwanja wa michezo. Akizungumzia mzozo huo meya wa Addis Ababa Afanech Abebe amesema: "Machafuko ni ya kundi Junta (TPLF) sio watu wa Tigray. Wapo Watigray wengi mjini Addis Ababa, ni ndugu zetu dada zetu. Hatua hii ya jeshi litawakomboa watu wa Tigray."

Watu wajitokeza kuchanga damu Addis Ababa kuwasaidia waathiriwa wa mgogoro wa Tigray
Watu wajitokeza kuchanga damu Addis Ababa kuwasaidia waathiriwa wa mgogoro wa TigrayPicha: Mulugeta Ayene/AP Photo/picture alliance

Ethiopia yamteua kiongozi mpya wa Tigray

Katika tukio jingine, bunge la Ethiopia limemteua kiongozi mpya wa jimbo la Tigray. Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed amesema hayo leo mnamo wakati vikosi vya serikali vikiendelea na mashambulizi dhidi ya viongozi wa jimbo hilo ambao serikali imewatuhumu kwa uhaini na ugaidi.

Tangazo hilo la Abiy Ahmed limejiri siku moja baada ya bunge kumuondolea kinga ya kushtakiwa, rais wa jimbo hilo Debretsion Gebremichael aliyechaguliwa Septemba, na ambaye pia ndiye mwenyekiti wa chama cha TPL.

Umoja wa Afrika wamfuta kazi mkuu wa usalama

Kando na hayo, Umoja wa Afrika umemfuta kazi mkuu wake wa usalama Gebreegziabher Mebratu Melese ambaye ni raia wa Ethiopia. Hii ni baada ya serikali ya Abiy Ahmed kumtuhumu Melese kwa kukosa uaminifu kwa taifa, mnamo wakati machafuko ya jimbo la Tigray yakitishia kuiyumbisha nchi hiyo ya pembe ya Afrika.

	Maelfu ya Waethiopia katika jimbo la Tigray wanakimbilia SUdan kufuatia machafuko.
Maelfu ya Waethiopia katika jimbo la Tigray wanakimbilia SUdan kufuatia machafuko.

Agizo la kuachishwa kazi kwa Melese limetolewa na Ofisi ya mkuu wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika yake Moussa Faki Mahamat, kufuatia barua ambayo shirika la habari la Reuters limeona, iliyoandikwa na jeshi la Ethiopia likielezea wasiwasi wake kuhusu uaminifu wa Melese. Umoja wa Afrika wataka mapigano yasitishwe Tigray.

Hata hivyo wizara ya ulinzi haikuzungumzia suala hilo moja kwa moja mapema leo.

Washukiwa 150 wakamatwa Addis kwa tuhuma ya ugaidi

Mgogoro wa Tigray ulianza Novemba 4, wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliamuru operesheni ya kijeshikufanywa akiwatuhumu viongozi wa jimbo hilo kwa kuagiza mashambulizi dhidi ya kambi ya kijeshi ya serikali kuu, na kuukaidi uongozi wake.

Mnamo Alhamisi, serikali ilisema iliwakamata wahalifu 150 wa chama cha TPLF mjini Addis Ababa na kwingineko ikishuku walikuwa wanapanga njama ya kufanya shambulizi la kigaidi.

(AFPE;RTRE)

Mwandishi: John Juma

Mhariri:  Gakuba, Daniel