Eritrea yajitoa kwenye jumuiya ya IGAD | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.04.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Eritrea yajitoa kwenye jumuiya ya IGAD

Eritrea imejiondoa kutoka kwenye jumuiya ya kutafuta amani ya eneo la Upembe wa Afrika - IGAD.

Rais Isaias Afewerki wa Eritrea

Rais Isaias Afewerki wa Eritrea

Wizara ya mambo ya nje ya Eritrea imesema katika taarifa yake kwamba imesimamisha uanachama wake kutoka kwenye jumuiya ya nchi saba - IGAD, yenye makao yake nchini Djibouti kutokana na kushindwa kwa jumuiya hiyo kupata suluhisho katika mzozo wa Somalia ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1000 na kuwalazimu maelfu ya raia wa Somalia kuihama nchi yao kufuatia vita baina ya majeshi ya Ethiopia na wapiganaji wa kiislamu tangu mwezi Januari.

Eritrea imedai pia kwamba jumuiya ya IGAD haizingatii amani na usalama wa eneo zima kwa jumla aidha mara kwa mara maazimio yasiyo na msingi yanayo bomoa na kudhoofisha amani na usalama wa eneo la Upembe wa Afrika yamepitishwa chini ya kivuli cha jumuiya ya IGAD imedai Eritrea.

Kujitoa huko kwa Eritrea kutoka kwenye jumuiya hiyo ya IGAD kunaashiria hali ya wasiwasi kati ya Asmara na hasimu wake wa muda mrefu Ethiopia kuhusu usimamizi katika mzozo wa Somalia.

Kwa sababu hizo serikali ya Eritrea imesema kwamba haitaki kuhusishwa katika maswala yatakayo itumbukiza serikali hiyo ndani ya migogoro ya kisheria na kibinadamu.

Eritrea taifa dogo lililo magharibi mwa bahari ya Sham lilijiunga na jumiya ya IGAD mnamo mwaka 1993.

Nchi wanachama wa jumuiya ya IGAD ni pamoja na Uganda, Sudan, Kenya Djibouti, Ethiopia na Somalia.

IGAD itakumbukwa kwa juhudi iliyotekeleza katika kutatua mzozo baina ya serikali ya Sudan na waasi wa zamani wa SPLM.

IGAD pia iliwezesha kupatikana serikali ya mpito ya Somalia mwaka 2004 ijapokuwa utawala huo umeshindwa kuidhibiti nchi nzima ya Somalia.

Lakini serikali ya Asmara imekuwa wakati wote inapingana na jumuiya ya IGAD tangu jumuiya hiyo ilipopitisha azimio la kupelekwa wanajeshi wa kulinda amani kwa ajili ya kuisaidia serikali ya mpito ya rais Abdullahi Yusuf Ahmed wa Somalia inayoungwa mkono na Ethiopia.

Wakati huo huo Eritrea imepinga Kenya kuingilia kati kama mpatanishi inailaumu nchi hiyo kwa kuipendelea Ethiopia na pia kwa kuuunga mkono uvamizi wa majeshi ya Ethiopia nchini Somalia.

Katika mkutano wa mawaziri wa IGAD mjini Nairobi mapema mwezi huu Ethiopia na Eritrea zilikwaruzana kuhusu kuwepo wanajeshi wa kigeni nchini Somalia na hali hiyo imeongeza mpasuko katika nchi masikini za eneo la Upembe wa Afrika.

Wachambuzi wameelezea wasiwasi wao juu ya kuendelea kuwepo kisasi baina ya Ethiopia na Eritrea kutokana na kutotatuliwa mzozo wa mipaka wa mwaka 1998 hadi 2000 na wanahofia kuwa nchi hizi mbili huenda zikaigeuza Somalia kuwa ndio uwanja wa kuminyana misuli.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com