Eritrea inatoa silaha kwa wapiganaji nchini Somalia,adai rais Sharif Ahmed. | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.05.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Eritrea inatoa silaha kwa wapiganaji nchini Somalia,adai rais Sharif Ahmed.

Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed amedai kuwa Eritrea inawapatia silaha wapiganaji wanaoipinga serikali yake.

Wapiganaji wa Kiislamu wakijiweka tayari kwa mapigano katika mitaa ya mjini Mogadishu.

Wapiganaji wa Kiislamu wakijiweka tayari kwa mapigano katika mitaa ya mjini Mogadishu.

Rais wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed ameishutumu Eritrea leo kwa kuwapa silaha waasi wa Kiislamu ambao wana nia ya kuiangusha serikali yake baada kuvurumishwa makombora dhidi ya makaazi yake mjini Mogadishu.Tunafahamu kwa hakika kuwa silaha nyingi zilizoko mikononi mwa wapiganaji zinatokea Eritrea, rais Sharif Sheikh Ahmed amewaambia waandishi habari wa kigeni mjini Mogadishu.

Eritrea inahusika sana hapa, amesema wakati akijibu swali na kuongeza kuwa tunafahamu kuwa maafisa wa Eritrea wamekuja hapa na kuleta fedha taslim.

Amesema kuwa nia ya Eritrea katika kuwaunga mkono Waislamu wenye imani kali ni kujenga ngome ambayo wapiganaji wanaoipinga Ethiopia watapata mafunzo na kuendesha mapigano ya chini kwa chini dhidi ya Addis Ababa.

Amesema pia kwa kuwa kuna vita na hali ya wasi wasi kati ya Ethiopia na Eritrea, Eritrea inahitaji sehemu ambapo makundi yanayoipinga Ethiopia yatapatiwa mafunzo.

Wanataka kuidhoofisha Ethiopia kutokea Somalia, ameongeza rais huyo katika mkutano huo na waandishi habari katika Villa Somalia, makao makuu ya rais ambayo yalikuwa lengo la mashambulizi ya wapiganaji siku ya Jumanne.

Uhusiano kati ya Ethiopia na Eritrea umekuwa wa wasi wasi muda mrefu tangu pale ilipozuka vita ya mpakani mwishoni mwa miaka ya 1990 ambapo mamia kwa maelfu ya watu waliuwawa.

Marekani pamoja na umoja wa Afrika wameishutumu Eritrea kwa kuchochea ghasia nchini Somalia, madai ambayo Eritrea inayakana. Mataifa ya Afrika yamekwenda umbali hata wa kutaka umoja wa mataifa kuiwekea vikwazo Eritrea.

Wapiganaji wa Somalia walianzisha mapigano mapya dhidi ya serikali ya mpito iliyo na umri wa miezi minne ya rais Sharif hapo Mei 7, na wameweza wakidhibiti maeneo kadha mjini Mogadishu katika mahandaki katika mtaa karibu na makaazi ya rais.

Tangu wakati huo mapigano yameongezeka na wapiganaji hao wa Kiislamu wameapa kuyaondoa majeshi ya serikali inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi katika taifa hilo la pembe ya Afrika.

Wakati zaidi ya watu 200 wamekwisha uwawa na kiasi cha watu wengine 62,000 wakaazi wa mjini Mogadishu wamekimbia makaazi yao katika muda wa siku 20 zilizopita, Sharif ameendelea kujificha katika jengo la makaazi yake ambalo lilishambuliwa tena siku ya Jumanne.

Siku ya Jumanne makombora ambayo yalilengwa katika makaazi ya rais Sharif yalikosa lengo lake na kupiga eneo la karibu la makaazi ya raia na kuuwa watu kadha. Analindwa na kiasi cha wanajeshi 4,300 wa jeshi la kulinda amani la umoja wa Afrika ambao wamewekwa March 2007.

Serikali ya mpito ya Somalia ambayo imekuwa ikidhibiti baadhi ya sehemu tu za mji mkuu Mogadishu , ilichukua madaraka Januari kufuatia hatua za mapatano zilizoendeshwa na umoja wa mataifa.

Lakini Waislamu wenye imani kali, wanaoaminiwa kuwa wanasaidiwa na mamia ya wapiganaji wa kigeni , wanataka kuweka sheria kali za Kiislamu, Sharia katika nchi hiyo ambayo haina sheria na wanapinga kuwapo kwa jeshi la kulinda amani la umoja wa Afrika , AMISOM.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa jana Jumanne lilirefusha muda wa kuwapo nchini Somalia kwa jeshi la AMISOM hadi Januari 2010.


Mwandishi Sekione Kitojo /AFPE

Mhariri : Abdul-Rahman

►◄
 • Tarehe 27.05.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HybB
 • Tarehe 27.05.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HybB
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com