1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan kukutana na Trump Jumanne

16 Mei 2017

Hatua ya jeshi la Marekani kuwaunga mkono waasi wa YPG, ndiyo itakayokuwa mada tete wakati rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan atakapokutana na rais Donald Trump katika ikulu ya White House Jumanne.

https://p.dw.com/p/2d2UP
Türkei Präsident Erdogan
Rais wa Uturuki Reccep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/A. Zemlianichenko/Pool

Wiki iliyopita Trump aliagiza wizara ya usalama ya Marekani, Pentagon, kulihami YPG nchini Syria katika vita vya kuliondoa kundi linalojiita Dola ya Kiislamu, IS, kutoka kwenye ngome yake ya al-Raqqa.

YPG ina usuhuba na Marekani ingawa Uturuki inaliona kundi hilo kama la kigaidi, lililo na uhusiano na wanamgambo wa Kikurdi PKK wanaopambana na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kusini mashariki mwa Uturuki. Inataka uamuzi wa Trump ubadilishwe na kikosi cha Uturuki ndicho kitumiwe katika vita hivyo.

Erdogan siku ya Ijumaa alieleza matumaini yake kwamba mkutano wake na Trump utatilia kikomo sera za kitambo.

YPG haina tofauti na PKK

Kundi la watu lilimkaribisha Erdogan alipowasili Washington usiku wa Jumatatu. Walikuwa wamebeba bendera za Uturuki huku wakilitaja jina la Erdogan karibu na White House.

"Marekani inastahili kuiamini Uturuki sasa," Nevzat Tuncel mwenye umri wa miaka 42 aliliambia shirika la habari la dpa, "Uturuki ni rafiki wa Marekani na NATO, lakini hatua ya Marekani kuliunga mkono YPG ni tatizo kubwa kwa Uturuki kwa  kuwa YPG haina tofauti na PKK. Unapolipatia YPG silaha, nusu ya silaha hizo zinakwenda kwa PKK."

USA Präsident Donald Trump im Weißen Haus
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Reuters/K. Lamarque

Msemaji katika wizara ya usalama ya Marekani Admiral James Davies alisema Jumatatu kwamba, maafisa wa Marekani wamefanya kila wawezalo kuihakikishia Uturuki kwamba, Marekani imejitolea kuzuia matatizo zaidi ya kiusalama na kuilinda Uturuki. Davies pia alisema kuwa, muungano wa Syrian Democratic Forces, ambao ni muungano wa Wakurdi wa Syria na Waarabu, ndilo kundi la pekee linaloweza kuichukua al-Raqqa, wakati wowote katika siku za usoni na kwamba YPG ni kiungo muhimu kwa SDF.

Suala la Fethullah Gulen huenda likaibuka

"Huenda wakaiteka tena al-Raqqa, ingawa kimsingi wanahitaji usaidizi ili waweze kufika mwisho," alisema Davies.

Katika mkutano wake wa Jumanne na Trump, Erdogan pia huenda akaibua lile suala la Fethullah Gulen, muhubiri wa Kituruki anayeishi uhamishoni nchini Marekani. Serikali ya Uturuki inadai Gulen alichangia katika jaribio la mapinduzi la mwaka jana na inataka kurejeshwa kwake nchini humo ili ahukumiwe. Uongozi uliopita wa Barack Obama ulikataa ombi hilo na ukataka kutolewe thibitisho.

Makundi yanayompinga Erdogan lakini yanapanga kufanya maandamano nje ya White House wakati wa ziara ya kiongozi huyo wa Uturuki.

Mwandishi: Jacob Safari/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga