1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Erdogan akiri changamoto kwenye shughuli za uokozi

Lilian Mtono
8 Februari 2023

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amekiri leo kwamba serikali yake ilikabiliwa na changamoto katika juhudi za awali za kukabiliana na athari za tetemeko kubwa lililoathiri eneo la kusini mwa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/4NFIV
Türkei | Präsident Recep Tayyip Erdogan in Kahramanmaras
Picha: Mustafa Kamaci /AA/picture alliance

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema hayo wakati kukiibuliwa malalamiko kutoka manusura waliogadhabishwa na hatua za taratibu za serikali za kuwafikishia vikosi vya uokozi. Watu zaidi ya 11,000 wanaripotiwa kufariki dunia hadi sasa kutokana na tetemeko hilo lililopiga Uturuki na Syria. 

Alisema "Ni kweli kulikuwa na matatizo siku ya kwanza, lakini baada ya hapo siku ya pili na hii leo hali ilirejea kawaida.. Lengo letu ni kujenga upya nyumba katika kipindi cha mwaka mmoja, kama tulivyofanya awali katika maeneo yaliyokumbwa na matetemeko ya ardhi, Kahramanmaras na majimbo mengine. Watu wetu hawapaswi kuwa na wasiwasi: hatukubali raia wetu yeyote kubaki mitaani."

Rais Recep Tayyip Erdogan anayewania muhula mwingine wa urais katika uchaguzi wa mwezi Mei, amesema wakati akiyazuru maeneo yaliyokumbwa na janga hilo.

Soma Zaidi: Tetemeko Uturuki na Syria: Waokoaji waendelea na kazi usiku kucha

Lakini wakati anasema hayo, wakazi katika maeneo ya kusini mwa Uturuki waliojitafutia makazi ya muda na vyakula hivi sasa wanakabiliwa na kadhia ya baridi kali wakiwa wanasubiri kwa machungu kuwaona ndugu ama jamaa zao wakati vikosi vya uokozi vikiendelea kuchimba wakiwasaka manusura, huku wengine wakitolewa wakiwa tayari wamefariki.

Türkei | Erdbeben Kahramanmaras Vater Opfer Trümmer
Mesut Hancer, mkazi wa Kahramanmaras nchini Uturuki akiwa amekaa karibu na bintiye aliyefariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi.Picha: Adem Altan/AFP/Getty Images

Hadi mchana wa leo, watu zaidi ya 11,000 waliripotiwa kufaridi dunia nchini Syria na Uturuki, wakati wasiwasi ukizidi kwamba huenda idadi hiyo ikaongezeka kwa kuwa majengo mengi yaliyoanguka huenda yakawa yamefukia watu waliokuwa wamelala wakati tetemeko hilo lilipotokea.

Wengi wa wakazi kwenye maeneo yaliyoathirika wameendelea kulala kwenye magari ama mitaani wakiwa wamejifunika mablanketi wakihofia kurudi kwenye majengo ambayo yana nyufa zilizotokana na tetemeko hilo. Familia nyingine kusini mwa Uturuki na Syria zimeendelea kupigwa na baridi kali kwa siku ya pili mfululizo kutokana na kukosa makazi.

Mmoja ya wakazi kwenye maeneo hayo amenukuliwa akilalama na kuhoji kulikoni hawajafikishiwa misaada kama ya mahema na vikosi vya uokozi. Akasema ni kweli wamenusurika na tetemeko, lakini sasa ni dhahiri watakufa kwa njaa ama baridi kali.

Soma Zaidi: Erdogan atangaza hali ya dharura katika maeneo ya tetemeko

Taarifa kutoka Beirut zinasema zaidi ya watu 298,000 wamelazimika kuondoka kwenye nyumba zao kutokana na tetemeko hilo, hii ikiwa ni kulingana na vyombo vya habari katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali na si yale yaliyoko chini ya tawala nyingine. Shirika la habari la serikali SANA limemnukuu waziri wa serikali za mitaa na mazingira Hussein Makhlouf akisema serikali pia imefungua maeneo 180 ya makazi kwa ajili ya watu walioondoka kwenye makazi yao.

Na kutoka huko Vatican, kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis ametuma salamu za pole kwa raia wa Uturuki na Syria kufuatia janga hilo. Amesema kwa huzuni nyingi anaziombea famili za wahanga na wale wote wanaoteseka kufuatia kadhia hiyo, huku akiutolea mwito ulimwengu kuendelea kuwaombea manusura wanaoanza kujipanga kuanza upya safari ya maisha.

Tizama zaidi: 

Jitihada za uokozi zinaendelea Uturuki,Syria