Eneo la mashariki la Mosul lakombolewa | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Eneo la mashariki la Mosul lakombolewa

 Waziri Mkuu wa Iraq  Haider al-Abadi  ametangaza rasmi kukombolewa upande wa mashariki wa  mji wa Mosul ambao hapo awali ulikuwa ukidhibitiwa na wanamgambo wa kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu (IS).

Vikosi vya Iraq vimefanikiwa kuwaondosha wanamgambo wa kundi hilo la Dola la Kiisilamu kutoka katika ngome yao ya mwisho katika eneo la mashariki la mji huo mnamo wakati mashirika ya misaada yakikadiria kiasi ya watu 750,000 bado wako katika eneo la magharibi la mji huo ambalo bado linadhibitiwa na wanamgambo wa IS.

Katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari Waziri Mkuu Haider al- Abadi alivisifu vikosi vyote vya usalama vilivyofanikisha operesheni hiyo pamoja na umma kwa kuunga mkono operesheni hiyo.

Mji wa Mosul ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq na ngome kuu ya mwisho ya kundi la Dola la Kiisilamu nchini Iraq uliangukia chini ya mikono ya kundi hilo wakati wa majira ya kiangazi mnamo mwaka 2014 wakati kundi hilo lilipoyashikilia  maeneo makubwa kaskazini na magharibi mwa Iraq.

Alipoulizwa na shirika la habari la Associated Press ni muda gani utahitajika ili kufanikisha kukomboa upande wa magharibi wa mji huo, al-Abadi alisema  hawezi kusema sasa lakini akaongeza kuwa wana uwezo wa kulikomboa eneo hilo na watafanya hivyo.

Mamia ya raia walilazimika kuyahama maeneo ya jirani ya kaskazini mashariki ya Rashidiya kwa miguu wakati helkopta za Iraq zilipolizunguka eneo hilo na kuwashambulia kwa mabomu wanamgambo wa IS.

Uchunguzi kufanyika dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu

Haider al-Abadi (C.Court/Getty Images)

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi

Wakati huohuo Waziri Mkuu Haider al- Abadi alirudia ahadi yake ya kufanya uchunguzi dhidi ya madai ya ukiukaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na vikosi vya Iraq na hatimaye kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote watakaobainika kuhusika.

Matamshi yake yanakuja  siku moja baada kuagiza kufanyika uchunguzi kuhusiana na vidio iliyoko katika mitandao ya kijamii inayoonyesha wanajeshi  wa vikosi vya serikali wakiwapiga na kuwaua watu watatu washukiwa wa kundi la Dola la Kiisilamu mjini Mosul.

Hapo jana kamati iliyoundwa kuchunguza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vilivyofanyika katika mji wa Fallujah Juni mwaka jana ilikamilisha kazi yake ambapo Waziri Mkuu al- Abadi alisema kamati hiyo imewahusisha wafuasi wa kundi la wanamgambo wa kishia  na mauaji ya raia 17.

Operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul ilianza Oktoba mwaka jana kwa msaada wa mashambulizi ya anga na ushauri kutoka muungano uanaoongozwa na Marekani. Hata hivyo Waziri Mkuu al- Abadi amekanusha kuwepo vikosi vya kigeni vinavyopambana  katika mashambulizi ya nchi kavu huku akisema utawala wa Rais wa sasa wa Marekani  Donald Trump  umeahidi kuongeza msaada wake kwa Iraq.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/DPAE

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com