Emmanuel Macron ahutubia bunge la Ulaya Strassbourg | Magazetini | DW | 18.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Emmanuel Macron ahutubia bunge la Ulaya Strassbourg

Hotuba ya rais wa Ufaransa katika bunge la Ulaya, juhudi za kusaka amani nchini Syria na uamuzi wa korti ya Ulaya dhidi ya utaratibu wa kuajiriwa watumishi wa mashirika ya makanisa Ujerumani magazetini

Tunaanzia katika bunge la Ulaya mjini Strassbourg ambako rais kijana wa Ufaransa jana alitoa hotuba ya kusisimua kuhimiza mageuzi ya umoja huo na kutahadharisha dhidi ya hisia kali za kizalendo. "Umoja wa Ulaya unazindukana" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaloendelea kuandika: "Kwa jinsi Emmanuel Macron alivyojitokeza mbele ya bunge la Ulaya mjini Strassbourg, mtu anaweza kusema kwa uhakika kabisa kwamba Umoja wa Ulaya unaweza kuchangamsha na kusisimua pia. Macron anajiona kama msanifu aliyedhamiria kuufanya uwe madhubuti Umoja wa Ulaya. Uwe madahubuti dhidi ya dharuba za migogoro ya fedha na pia dhidi ya hisia kali za kizalendo zilizoenea vichwani mwa baadhi ya viongozi. Hatua kadhaa alizozitetea aliwahi kuzizungumzia katika hotuba yake katika chuo kikuu cha Sorbonne mjini Paris miezi sita iliyopita. Hadi wakati huu lakini hakuna aliyegutuka. Hakuna yeyote miongoni mwa wanachama anaetaka kukamata mwiko wa mwasi na kuanza ujenzi wa umoja mpya wa ulaya. Lakini Emmanuel Macron hakati tamaa. Anaelekeza macho mbali zaidi badala ya kuukodolea mstari mwekundu. Ukakamavu wake unastahiki sifa. Ameshasema katika hotuba yake ya Sorbonne atafuata uzi huo huo. Na ni bora hivyo kwasababu Umoja wa ulaya unahitaji kiongozi ambae hakubali kuvunjwa moyo."

Nani wa kuongoza mazungumzo ya amani Syria?

Nchini Syria baada ya hujuma za kijeshi zilizoongozwa na Marekani na kuzihusisha pia  Ufaransa na Uingereza, kauli mbiu sasa ni kufufua juhudi za amani. Suala gazeti la "Der Tagesspiegel" linalojiuliza, juhudi hizo ziongozwe na nani? Gazeti linaendelea kuandika: "Serikali kuu ya Ujerumani imeshasema hakuna mazungumzo yatakayoweza kufanyika bila ya kumhusisha kiongozi wa nchi hiyo. Lakini nani wa kuongoza mazungumzo hayo? Kutokana na hali namna ilivyo, kansela Merkel ndie anaebidi kujitosa katika bahari hiyo. Bashar al Assad hataki kuzungumza  wala kujadiliana na wale wote waliohusika na hujuma za kijeshi. Wakati huo huo ni sawa pia kwamba juhudi hizo zitabidi zishughulikie pia kipindi cha mpito cha baada ya Assad. Chochote chengine kitazichafulia hadhi nchi za magharibi. Ufumbuzi wa kudumu unawezekana nchini Syria  bila ya Assad. Suala hapo vipi Assad anaweza kutanabahishwa kuhusu ukweli huo? Bila ya shaka duru moja ya mazungumzo haitotosha na bila ya shaka haitowezekana bila ya kuzihusisha Urusi, Saudi Arabia na Iran. Na nani wa kuzungumza nao? Changamoto kubwa zinamsubiri kansela Angela Merkel pindi akikubali kuwa mpatanishi."

Uamuzi wa korti ya Ulaya

Mada yetu ya mwisho inahusu uamuzi wa korti ya ulaya mjini Luxemburg kuhusu muongozo wa kuajiriwa watumishi wa mashirika yanayomilikiwa na kanisa. Hadi wakati huu mwajiriwa wa taasisi kama hizo alilazimika kuwa muumini. Korti ya Ulaya inasema mwongozo huo si wa haki na kudai milango ya ajira iwe wazi kwa wote.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com