1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EL-GENEINA : Majeshi 100,000 hayawezi kuleta amani Dafur

25 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC7Q

Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa amesema hata kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani 100,000 hakiwezi kuleta amani katika jimbo la Dafur nchini Sudan.

Antonio Guterres amesema ni ufumbuzi kababambe tu wa kisiasa kwa mgogoro huo ndio utakaoweza kukomesha mzozo wa miaka minne huko Dafur ambapo Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba watu 200,000 wamekufa na wengine milioni mbili na nusu wamepotezewa makaazi yao.

Akizungumza katika mkutano na masheik wa watu waliopoteza makaazi yao katika kambi ya Krinding huko El-Geneina mji mkuu wa jimbo la Dafur ya magharibi amesema bila ya amani hakuna miujiza na kwamba hakuna kikosi cha usalama kitakachoweza kuhakikisha kuwepo kwa usalama kwa jimbo lote la Dafur ambalo amesema ni kubwa sana.

Sudan hivi karibuni ilikubali mpango mkubwa wa msaada kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika walioko Dafur kwa kujumuisha wanajeshi na polisi 3,500 hata hivyo imekataa dai la Umoja wa Mataifa la kuruhusu wanajeshi 20,000 kulinda amani huko Dafur.