1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola kuendelea kusababisha maafa zaidi magharibi mwa Afrika

Ricardo von Beck4 Julai 2014

Shirika la Afya la Duniani WHO limesema kuwa mripuko wa ugonjwa wa Ebola uliozuka katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi utaendelea kuwaathiri na kusababisha vifo zaidi kwa kipindi cha miezi kadhaa ijayo

https://p.dw.com/p/1CVdk
Picha: Reuters

Ugonjwa huo unaoenea kwa kasi kwa kuambukizwa na kirusi kinachopatikana katika ukanda wa nchi za joto hadi sasa umeshawaathiri mamia ya watu katika nchi za Guinea, Liberia, na Sierra Leone ambako kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za WHO, idadi ya watu waliopoteza maisha ambao wamethibitishwa au kuhisiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo inafikia 467, na wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo unaweza ukaenea katika ukanda wote wa magharibi mwa Afrika.

Akifunga mkutano huo uliofanyika mjini Accra, Ghana, na kuwashirikisha mawaziri wa afya kutoka nchi za Afrika Magharibi, mkurugenzi msaidizi wa usalama wa afya wa WHO, Keiji Fukuda, amesema kwa sasa ni vigumu sana kutoa jibu la wazi ni jinsi gani ugonjwa unaweza ukaenea au ni lini utatokomezwa.

MSF yatoa tahadhari

"Nina matumaini sote tutaona kuona mabadiliko ya kupungua kwa matukio katika wiki kadhaa zijazo" alisema Fukuda wakati wa mkutano huo.

Wahudumu wa afya wakimuhudumia mgonjwa wa Ebola Sierra Leone
Wahudumu wa afya wakimuhudumia mgonjwa wa Ebola Sierra LeonePicha: Reuters

Marie-Christine Ferir ambaye ni daktari kutoka shirika la madaktari wasio na mipaka(MSF) anasema mlipuko wa ugonjwa huo utaendelea kwa wiki kadhaa na pengine miezi katika baadhi ya maeneo.

Naye Waziri wa Afya wa Liberia Bernice Dahn anaamini kwa namna moja au nyingine mkutano huo wa Accra utawasaidia katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola

Mawaziri wa afya wakutana kuhusu Ebola

Abdulsalami Nasidi anayetokea katika kituo cha kukabiliana na ugonjwa wa ebola nchini Nigeria anasema wamekubaliana kwa pamoja kutoa elimu kwa viongozi wa vijiji juu ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kusaidiana na madaktari ambao wapo katika maeneo yao.

Afisa wa UNICEF akihamasisha umma kuhusu Ebola Liberia
Afisa wa UNICEF akihamasisha umma kuhusu Ebola LiberiaPicha: picture-alliance/dpa

Kutokana na kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo wa Ebola katika baadhi ya mataifa ya magharibi mwa Afrika, mawaziri wa afya kutoka nchi 12 walikutana katika mkutano wa siku mbili uliofanyika mjini Accra Ghana kujadili ni kwa jinsi gani wanaweza wakakabiliana na ugonjwa huo.

Aidha mawaziri hao, walitarajiwa kutoa mapendekezo kwa serikali za kanda wanazotokea katika kukabiliana na Ebola pamoja na kuzindua mpango wa kupiga vita ugonjwa huo ambao unagharimu dola millioni 10 za Marekani.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO, kabla ya mripuko huu wa sasa, ugonjwa wa Ebola umesababisha vifo vya watu wapatao 1,587.

Mwandishi: Anuary Mkama/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef