Ebola kudhibitiwa ifikapo 2015 | Matukio ya Afrika | DW | 07.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Ebola kudhibitiwa ifikapo 2015

Viongozi wa mataifa ya jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, wamemchagua rais wa Togo kuongoza vita dhidi ya Ebola. Umoja wa Mataifa umesema ugonjwa huo unaweza kudhibitiwa ifikapo 2015.

Katika mkutano wao wa dharura unaofanyika mjini Accra, Ghana, viongozi wa ECOWAS wamempa rais Faure Gnassingbe wa Togo jukumu kubwa la kusimamia juhudi za kudhibiti kusambaa virusi vya Ebola katika eneo la Afrika Magharibi. Ugonjwa huo mpaka sasa umewaua watu wapatao 5,000 na inakadiriwa zaidi ya watu 13,000 wameambukizwa virusi.

ECOWAS imeyataka mashirika ya misaada yatoe kipaumbele kwa usambazaji wa chanjo ya bei nafuu dhidi ya Ebola. Rais John Mahama wa Ghana amekumbusha kwamba nchi zilizoathirika lazima zitumie wakati huu kuimarisha huduma za afya. Aliongezea kwamba nchi mwanachama wa ECOWAS zimeahidi kufanya kila juhudi kuhakikisha wanaushinda ugonjwa wa Ebola.

Japan yatoa dola milioni 100

Mratibu wa juhudi za Umoja wa Mataifa kupambana na Ebola, David Nabarro

Mratibu wa juhudi za Umoja wa Mataifa kupambana na Ebola, David Nabarro

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa na matumaini ya uwezekano wa Ebola kudhibitiwa ifikapo mwaka ujao. Hayo yamesemwa na Daktari David Nabarro, mratibu wa juhudi za Umoja wa Mataifa za kupambana na Ebola. Hata hivyo Nabarro ameonya kuwa bado ipo kazi kubwa ya kufanya. "Katika baadhi ya maeneo kasi ya maambukizi imepungua," amesema Nabarro. "Lakini siwezi kusema kwamba tumeshinda vita hivi mpaka pale ambapo mgonjwa wa mwisho atakuwa anatibiwa. Hadi wakati huo lazima tuwe makini sana. Hali bado ni mbaya."

Nabarro aliisifu jumuiya ya kimataifa kwa utayari wa kushiriki katika mapambano dhidi ya Ebola. Amesema idadi ya vitanda vya kuwalaza wagonjwa kwenye nchi zenye visa vingi zaidi vya Ebola, imeongezeka mara tatu ndani ya miezi miwili. Hata hivyo, daktari huyo ameeleza kuwa fedha nyingi zaidi zinahitajika kutoka kwa nchi na mashirika mbali mbali. "Ingawa tumepokea fedha nyingi za misaada, fedha hizo bado haitoshi. Pamoja na hayo, tumeongeza kisio la kiasi kinachohitajika. Badala ya dola bilioni moja sasa tunahitaji dola bilioni moja na nusu," amesema Nabarro.

Miongoni mwa mataifa yanayochangia kiasi kikubwa cha fedha ni Japan ambayo imetangaza kwamba itatoa hadi dola za kimarekani milioni 100 kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Ebola Afrika Magharibi. Tangazo la Japan limekuja baada ya rais Obama wa Marekani kuihimiza jumuiya ya kimataifa kushirikiana ili kutoa zaidi ya dola bilioni 6 kama msaada wa dharura kwa nchi zilizoathirika zaidi. Mwezi Septemba mwaka huu, waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, tayari alikuwa ameahidi kuchangia dola milioni 40.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/reuters/ap

Mhariri: Saumu Yusuf