1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DW yakanusha kuingilia masuala ya ndani ya Urusi

Saumu Mwasimba
5 Septemba 2019

Urusi inatishia kubatilisha kibali cha Deutsche Welle baada ya kukataa  mwaliko wa kufika mbele ya tume ya bunge la Urusi mjini Moscow. Urusi inadai DW imeshawishi wananchi wake waandamane

https://p.dw.com/p/3P6hL
DW-Intendant Peter Limbourg
Mkurugenzi mkuu wa DW Peter Limbourg Picha: DW/M. Magunia

Urusi inatishia kubatilisha kibali cha Deutsche Welle baada ya kukataa  mwaliko wa kufika mbele ya tume ya bunge la Urusi mjini Moscow. Mkurugenzi mkuu wa Dw Peter Limbourg ameyakanusha madai yanayotolewa na Urusi.

Katika taarifa ya DW, Peter Limbourg ameyapinga madai ya Urusi kwamba DW imeingilia kati masuala ya ndani ya Urusi. Urusi inaituhumu DW kwa kutumia ujumbe wa Twita kuwatolea mwito wananchi wake washiriki kwenye maandamano yaliyopigwa marufuku.

Ujumbe huo uliokuwa umeandikwa kwa lugha ya Kirusi DW iliripoti juu ya maandamano yaliyozuiwa mjini Moscow na kunukuu mojawapo ya  maneno yaliyokuwa yakiimbwa  na waandamanaji. Katika taarifa yake ya kujibu mwaliko kutoka bunge la Urusi, Duma, DW imesema ''Ripoti zetu zinazingatia kanuni za uandishi wenye usawa. Kanuni hizo hazihusiana na kuingilia masuala ya ndani ya nchi yoyote ile''

Kadhalika Limbourg amemwambia kiongozi wa jopo la uchunguzi la Duma,Vasily Piskaryov kwamba, ''Siku zote tuko tayari kwa majadiliano na tumemualika bwana Piskaryov, lakini tunapaswa kukubaliana kuhusu muundo wa majadiliano. Hatua hii ya kutuita kwa hakika sio njia mwafaka kwa mazungumzo.''

Katika maelezo hayo Limbourg ameeleza kuwa kitisho cha kubatilisha kibali cha DW kinaonesha sura ya mwaliko huu.

''Sisi ni chombo huru cha matangazo na hatutokubali kuhujumiwa. Mbali na hilo, tumeweka wazi mara kadhaa kwamba hatukuhusika na kuingilia masuala ya ndani ya Urusi na wala hatutodiriki kufanya hivyo siku zijazo.'' Ameeleza mkurugenzi mkuu wa DW katika ujumbe wake kwa Piskaryov.

Peter Limbourg amesema DW haijawahi kutowa mwito wa maandamano kupitia ujumbe wa twitta, akifafanua kuwa ''tulichofanya ni kunukuu tu walichosema waandaaji wa maandamano.''

''Kwa sababu hili liko wazi,hatuwezi kuelewa sokomoko lote hili. Tuhuma kwamba DW imekiuka sheria za Urusi hazina msingi.'' Amemalizia Limbourg.

Mwandishi:Martin Muno/Saumu Yusuf

Mhariri:Daniel Gakuba