DW limezindua televesheni yake kwa lugha ya Kiingereza | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 22.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

DW limezindua televesheni yake kwa lugha ya Kiingereza

Shirika la Utangazaji la DW leo limezindua televisheni yake itakayotangaza kwa saa 24 kwa lugha ya Kiirengeza. Uzinduzi huo umefanyika siku ya kwanza ya Kongamano la nane la kimataifa la vyombo vya habari.

Saa tano kamili saa za hapa Ujerumani mkurugenzi Mtendaji wa Deutsche Welle, Peter Limbourg amezindua rasmi televesheni hiyo inayotangazia moja kwa moja kutoka mji mkuu Berlin akisema "Kama taifa la demokrasia katikati mwa Ulaya, tunataka maadili ya Ulaya yaeleweke zaidi na kukubalika na watu wengi ulimwenguni. Uzinduzi wa televisheni yetu kwa lugha ya Kiingereza ni hatua muhimu kuelekea kuifikia azma hiyo."

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano la kimataifa la vyombo vya habari, Limbourg amesema teknolojia inakua kwa kasi kubwa kote ulimwenguni na matumizi ya mtandao wa mawasiliano wa intaneti na mitandao ya kijamii yameenea katika maeneo ambayo kitamaduni yamekuwa yakitumia redio kama njia pekee ya kupata habari. Mkurugenzi huyo amesema uhuru wa vyombo vya habari umeendelea kubanwa katika sehemu mbalimbali za dunia huku waandishi wakikandamizwa na mifumo ya kisiasa na maisha yao kufuatiliwa."Uandishi na utangazaji wa habari unaendelea kuwa vigumu kuutekeleza. Mara nyingine ni kutokana na kukosa uelewa na ujuzi kuhusu taaluma hii na wakati mwingine ni kutokana na ukosefu wa fedha. Lakini mara nyingi kuzorota kwa taaluma hii ni sababu za kisiasa," amesema Limbourg.

Limbourg aidha amesema huku ufanisi katika upashahji habari ukiendelea kukua, uhuru wa vyombo vya habari haukui na kutoa mwito hatua za makusudi zichukuliwe kuhakikisha uhuru huo unalindwa na kuendelezwa. Amesema muundo mpya wa televesheni ya DW umeandaliwa mahususi kwa ajili ya mashujaa katika jamii wanaotegemea mawazo ya kimataifa kutoa mchango mkubwa katika maeneo wanakoishi. Hawa ni watu wanaofikiri, wanaotafakari, wavumbuzi, wanaohimiza wengine kusonga mbele katika juhudi za maendeleo badala ya kuwa vikwazo.

Bwana Limbourg ameshirikiana na Waziri wa utamaduni na vyombo vya habari wa Ujerumani, Monika Grütters, kuifungua rasmi televisheni hiyo. Bi Grütters amesema viongozi wa kisiasa wana jukumu kukikabili kitisho cha kufuatiliwa kwa taarifa binafsi za watu na uhuru wao kuingiliwa kutokana na mifumo ya sasa mawasiliano ya digitali."Wazo ni kuyahifadhi maadili tunayoyaona kuwa ya msingi wa demokrasia yetu katika ulimwengu huu wa mfumo wa analojia na maisha ya digitali, na kuyalinda."

Kongamano la mwaka huu limewaleta pamoja wajumbe takriban 2,000, kutoka nchi zaidi ya 100 wengi wao wakiwa ni waandishi wa habari. Miongoni mwa mada zitakazoangaziwa ni sera ya kigeni na kutipoti kuhusu mizozo ya kimataifa, njia za kuulinda uhuru wa kutoa maoni, uhalifu katika mitandao ya kijamii na vita vya jihad.

Mwandishi:Josephat Charo

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com