Duru ya pili ya uchaguzi wa mchujo Ufaransa | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Duru ya pili ya uchaguzi wa mchujo Ufaransa

Mamilioni ya wapiga kura wa Ufaransa wanateremka vituoni kutoa sauti zao kumchagua atakaekuwa mgombea wa chama cha kihafidhina, Les Republicains,uchagizi wa rais utakapoitishwa mapema mwakani.

 

Waziri mkuu wa zamani Francois Fillon anapewa nafasi nzuri ya kushinda na kushindana na rais anaemaliza wadhifa wake Francois Hollande na mgombea wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia,Marine Le Pen uchaguzi wa rais utakapoitishwa mwakani.

Zoezi la  uchaguzi wa mchujo,ambalo ni mfano wa lile la Marekani,ni la kwanza kwa chama cha kihafidhina cha Ufaransa Les Republicains na limegeuka kuwa pambano kali kati ya mhafidhina anaefuata sera kali za kiuchumi na mfuasi wa siasa za wastani Alain Juppé aliyewahi pia kuwa waziri mkuu wa Ufaransa.

Uchaguzi wa rais nchini Ufaransa unaangaliwa kama mtihani kwa vyama vikuu vya kisiasa hasa baada ya Donald Trump kuzusha maajabu kwa kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani na pia baada ya kura ya Brexit ya Uingereza.

Vituo vya kupiga kura vimefunguliwa tangu saa mbili asubuhi kwa saa za Ulaya ya kati-kila mpiga kura anatakiwa alipe Euro mbili kuweza kuruhusiwa kumchagua mgombea wabaemtaka.

Wapiga kura wanaendelea kutoa sauti zao

Wapiga kura wanaendelea kutoa sauti zao

Idadi ya wapiga kura imepindukia ile ya wiki iliyopita

Saa sita za mchana zaidi ya wapiga kura milioni moja na laki mbili walikuwa wameshapiga kura -hilo likiwa aongezeka la asili mia 13 ikilinganishwa na idadi ya walioteremka vituoni duru ya kwanza ya uchaguzi wa mchujo ilipoitishwa jumapili iliyopita.

Fillon aliyewahi kuwa waziri mkuu wakati wa utawala wa Nicolas Sarkozy kati ya mwaka 2007 hadi 2012 anaonya "Ufaransa imefikia ukingoni mwa janga la uasi" akiamini mpango wake wa kufutilia mbali nafasi laki tano za kazi miongoni mwa watumishi wa serikali na kuzifanyia marekebisho ya kina sera za kiuchumi itasaidia kuikwamua nchi hiyo.

Nitafanya kila niwezalo kwaajili ya wajasiria mali" alisema katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni ya uchaguzi ijumaa iliyopita mjini Paris akiahidi kuwasaidia matajiri kubuni nafasi za kazi ili kupunguza idadi ya wasiokuwa na ajira wanaokadiriwa kufikia asili mia 10 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini humo.

Francois Fillon baada ya kupiga kura

Francois Fillon baada ya kupiga kura

Waislam wanabidi wakubali kufuata kile ambacho dini nyengine zimekubali kufuata tangu zamani kufuata Ufaransa

Fillon anaungwa mkono pia kutokana na msimamo wake mkali pia kuelekea wahamiaji wa kiislam pamoja na kusisitiza umuhimu wa kulindwa kitambulisho cha wafaransa,lugha na maadili ya familia. Katika hotuba yake ijumaa iliyopita mjini Paris,Fillon amesema "dini ya kiislam inabidi ifuate kile ambacho dini zote nyengine zilikiridhia tangu zamani...na kwamba itikadi kali na uchokozi havina nafasi nchini humo."

Alain Juppé anamtuhumu mpinzani wake kutaka "kuleta mageuzi makali" na kwamba mpango wake ambao "hautekelezeki"unaungwa mkono na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.

Alain Juppé anaepigania pia mageuzi na kuipunguzia Ufaransa mzigo wa madeni ameahidi kuhakikisha jamii inaishi kwa "furaha na masikilizano" licha ya mchanganyiko wa tamaduni tofauti na  wasi wasi wa kitisho cha wahamiaji na itikadi kali.Anaesema yeye peke yake ndie atakaeweza kumshinda Marine Le Pen uchaguzi wa rais utakapoitishwa mwakani.

Yeyote atakaeibuka na ushindi wa uchaguizi wa mchujo wa wahafidhina,atashindana pia na rais anaemaliza mhula wake Francois Hollande anaedhihirika amepania kuisafisha hjadhi yake inayozidi kuchujuka.Uchunguzi wa maoni ya wananchi unaonyesha hata hivyo waziri mkuu Manuell Valls atakuwa mgombea abora zaidi kuliko Hollande.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Zainab Aziz

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com