1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaungana na Ukraine kuilaani Urusi

Mohammed Khelef
24 Februari 2023

Viongozi wa mataifa mbalimbali ulimwenguni wameuzungumzia mwaka mmoja wa vita vya Urusi nchini Ukraine wakionesha uungaji mkono wao kwa Ukraine na kutaka kukomeshwa kwa uvamizi huo mara moja.

https://p.dw.com/p/4NwWu
Belgien | NATO | Treffen Jens Stoltenberg mit Dmytro Kuleba und Josep Borrell
Picha: Johanna Geron/REUTERS

Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, Jens Stolenberg, amesema raia wa Ukraine watashinda kwenye vita vyao dhidi ya Urusi mwaka mmoja tangu uvamizi wa tarehe 24 Februari 2022.

"Uhuru hauko uhuru, lazima tuupiganie kila siku. Leo watu wa Ukraine wanapigania uhuru wao kishujaa na licha ya mwaka mzima wa fadhaa na uharibifu, dhamira na ujasiri wao utashinda." Alisema mkuu huyo wa NATO.

Kwa upande wake, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema Rais Vladimir Putin wa Urusi ameshindwa kufanikisha hata lengo moja.

Mwaka mmoja tangu Urusi kuivamia Ukraine

"Mwaka mmoja tangu kuanzisha vita vyake vya kikatili, Putin ameshindwa kufikia chochote katika malengo yake ya kimkakati. Badala yake ya kuifuta Ukraine kutoka ramani ya dunia, amekumbana na taifa ambalo liko imara zaidi kuliko awali." Alisema mkuu huyo wa Umoja wa Ulaya.

Vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida, alisema kwenye mkutano wa kundi la mataifa saba tajiri duniani kwamba watatoa wito wa kusitishwa kwa utumwaji msaada wa kijeshi kwa Urusi pamoja na kujadiliana vikwazo vipya dhidi ya Moscow.

Präsident Wladimir Putin nimmt an Kranzniederlegung teil
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Mikhail Metzel/Sputnik/AFP

Kwa upande wake, Marekani imetangaza awamu nyengine ya vikwazo yenye lengo la kuzidisha machungu ya kiuchumi kwa Urusi.

Vikwazo hivyo vipya, ambavyo vinazilenga taasisi mahsusi kama vile benki, madini, na sekta ya ulinzi, vitazihusu kampuni na watu 200, raia wa Urusi na kutoka mataifa mengine ya Ulaya, Asia,  na Mashariki ya Kati yanayounga mkono vita vya Urusi nchini Ukraine, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Marekani.

Mfalme Charles wa Pili wa Uingereza ametumia ujumbe wake wa leo kulaani kile alichokiita "mashambulizi yasiyokuwa na sababu dhidi ya Ukraine", akiongeza: "Sasa umetimia mwaka mmoja ambapo watu wa Ukraine wanateseka kwa kiwango kisichofikirika kutokana na mashambulizi dhidi ya taifa lao. Dunia imeyaona maovu na mateso haya, na tunasimama pamoja nao." 

Soma zaidi: Zelensky aapa Ukraine kuishinda Urusi, NATO kuzidisha misaada
Baraza kuu la UN laitaka Urusi kuondoa majeshi yake Ukraine

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amerejelea msimamo wa nchi yake kuiunga mkono Ukraine, akiwalenga moja kwa moja raia wanaokumbwa na machungu makali ya vita hivi kwa kuwaambia: "Watu wa Ukraine, Ufaransa iko upande wenu. Kwa mshikamano. Kwa ushindi. Kwa amani."

Ujerumani, inayohudhuria mkutano wa mawaziri wa fedha wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani unaofanyika Bengaluru nchini India, imetaka tamko la pamoja la mkutano huo lazima litaje neno "vita", kufuatia taarifa kwamba mwenyeji India inataka kuepukwa kutumia neno hilo.

Chanzo: AFP