Dunia yaukaribisha Mwaka Mpya | Masuala ya Jamii | DW | 01.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Dunia yaukaribisha Mwaka Mpya

Dunia imeukaribisha mwaka mpya wa 2014 kwa fataki, chereko, shangwe kubwa na kutakiana kheri. Sherehe kubwa zilizofanyika Dubai na mji mkuu wa Ujerumani, Berlin ni mfano wa zile zilizotia fora.

Fataki zikimeremeta juu ya anga la Dubai (01.01.2014).

Fataki zikimeremeta juu ya anga la Dubai (01.01.2014).

Dubai imevunja rekodi ya dunia kwa maonyesho makubwa kabisa ya fataki kuwahi kushuhudiwa katika Mkesha wa Mwaka Mpya yaliyohusisha fashifashi nusu milioni.

Fataki hizo zilin'gara angani kwa dakika sita na kutanda kwenye mwambao wa Dubai wa kilomita 100, kivutio kikuu cha fataki hizo kikikiwa kutoka kwenye jumba refu kabisa duniani la Burj Khalifa lenye urefu wa mita 830 na katika hoteli ya kifahari ya Atlantis ilioko Palm Jumeira, mojawapo ya visiwa vitatu vilivyotengenezwa na binaadamu kikiwa na umbo la mtende.

Rikodi ya mwisho iliwekwa na Kuwait hapo mwaka 2011 kwa onyesho la fataki 77,282 lililodumu kwa saa nzima.

Berlin kumen'gara

Baada ya kuingia kwa mwaka mpya Berlin.(01.01.2014).

Baada ya kuingia kwa mwaka mpya Berlin.(01.01.2014).

Wananchi wa Ujerumani wameukaribisha mwaka mpya kwa onyesho kubwa la fataki na vifijo ambapo tafrija kubwa kabisa ililifanyika mjini Berlin katika Lango la Brandenburg ambapo mamia kwa maelfu walihesabu kwa pamoja dakika za lala salama kabla ya kuingia mwaka mpya.

Milango ya kuingia kwenye eneo la tafrija hiyo ilibidi kufungwa na mapema kutokana na umma mkubwa uliofurika kuhudhuria tafrija hiyo ambapo inakadiriwa kwamba watu milioni mbili walimiminika mjini humo kwa ajili ya sherehe hiyo ya kuaga mwaka na kukurabisha mwaka mpya.

Mambo yalivyokuwa London wakati wa kuingia kwa mwaka mpya.(01.01.2014).

Mambo yalivyokuwa London wakati wa kuingia kwa mwaka mpya.(01.01.2014).

Mjini London ambapo mwaka mpya umeingia saa moja baada ya kupokelewa nchini Ujerumani takriban watu 50,000 waliushangilia kwa maonyesho ya fataki kwenye kingo za Mto Thames wakati kengele ya saa kuu ilioko kwenye la jengo la bunge la nchi hiyo mjini London ikihanikiza ilipotimia sita za usiku kuashiria kuingia kwa mwaka mpya.

Tafauti za wakati

Sherehe za mwaka mpya mjini Moscow.(01.01.2014).

Sherehe za mwaka mpya mjini Moscow.(01.01.2014).

Nchini Urusi maelfu ya watu wameukaribisha mwaka mpya kwa onyesho la fataki katika uwanja wa "Red Square" mjini Moscow lakini kwa desturi kutokana na kupishana kwa wakati katika majimbo mengi ya Urusi watu hawaukaribishi mwaka huu kwa wakati mmoja na kengele ya kuingia kwa mwaka mpya hulia kwenye saa ya Mnara wa Ikulu ya Kremlin tarehe 1 Januari.

Kutokana na mashambulizi ya kigaidi katika mji wa Volgograd miji mingi nchini Urusi imeimarisha usalama au kufuta kabisa sherehe za mwaka mpya.

Mbingu za pwani ya Copacabana huko Rio de Janeiro,Brazil zili'ngaa wakati wa mwaka mpya.(01.01.2014)

Mbingu za pwani ya Copacabana huko Rio de Janeiro,Brazil zili'ngaa wakati wa mwaka mpya.(01.01.2014)

Watu wanaofikia milioni mbili na laki tatu wamejimwaga katika pwani mashuhuri ya Copacabana mjini Rio de Janeiro nchini Brazil kuukaribisha mwaka mpya kwa maonyesho ya tani 24 za fataki na muziki wakati nchi hiyo mwaka huu ikiwa mwenyeji wa michuano ya soka kuwania Kombe la Dunia.

Visiwa vya Kiribati na Samoa huko Pasifiki vilikuwa vya kwanza kuushuhudia mwaka mpya duniani ikifuatiwa na New Zealand kabla ya watu milioni 1.6 katika bandari ya Sydney nchini Australia ambao ni mji mkubwa kabisa nchini humo kuukaribisha mwaka huo kama kawaida kwa onyesho la shani la tani saba za fataki katika fukwe za Jengo la Opera.

Hawakujali baridi

Mjini New York watu wanaokadiriwa kufikia milioni moja wakivumilia baridi kali na baadhi yao wakiwa wamepiga kambi tokea asubuhi kwa ajili ya kujipatia nafasi nzuri ya kujionea shamra shamra za kuukaribisha mwaka mpya walihesabu kwa sauti moja dakika za mwisho kuingia mwaka mpya.

Sherehe za mwaka mpya mjini New York.(01.01.2014).

Sherehe za mwaka mpya mjini New York.(01.01.2014).

Vipaza sauti vilihanikiza kwa wimbo wa kitambulisho wa Frank Sinatra "New York, New York" katika dakika za kwanza za kuanza kwa mwaka mpya na wanaanga watatu wa anga za juu kutoka Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu walijitokeza kwenye kioo kikubwa cha Televisheni kuutakia umati uliofurika hapo heri ya mwaka mpya.

Visiwa vya mbali vya Marekani vya Howland na Baker vitakuwa vya mwisho kuukaribisha mwaka mpya.

Asia yazingatia mila

Nchini Japani mamilioni ya watu wamezuru mahekalu kuukaribisha mwaka mpya kwa tafakuri na kuombeana dua.

Mjini Seoul Korea Kusini kengele ya shaba ya karne ya 15 imepigwa mara 33 kwa kuzingatia mila ya kale ya mwaka mpya.

Nchini Indonesia ngome kuu ya Sharia ya Kiislamu Banda Aceh sherehe za mwaka mpya zimepigwa marufuku kwa mara ya kwanza huku polisi wa itikadi kali za Kiislamu wakitaifisha maelfu ya fataki na matarumbeta yaliokuwa yatumike kuukaribisha mwaka.

Picha ya Hayati Nelson Mandela zimetanda kila pembe ya dunia.

Picha ya Hayati Nelson Mandela zimetanda kila pembe ya dunia.

Afrika ya Kusini nayo imeuaga mwaka 2013 kwa video ya kumuaga hayati Nelson Mandela wakati nchi hiyo ikianza mwaka mpya bila ya kuwa na shujaa wao huyo kipenzi.

Sura ya Mandela, rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo, imetanda kwenye ukumbi wa jiji wa Cape Town ambapo hapo mwaka 1990 alitowa hotuba yake ya kwanza baada ya kuwa kifungoni kwa miaka 27 chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa/afp/ap

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com