Dunia yatakiwa kulinda raia wa Dafur | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 12.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Dunia yatakiwa kulinda raia wa Dafur

Timu ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa leo hii imesema kwamba dunia ina wajibu wa dharura kuwalinda raia huko Dafur dhidi ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu ambapo kwayo serikali ya Sudan inatimiza dhima kubwa katika uhalifu huo.

Wakimbizi wa Dafur.

Wakimbizi wa Dafur.

Timu hiyo iliokuwa ikiongozwa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Jody Williams imesema serikali ya Sudan imeshindwa kuwalinda watu wa Dafur kutokana na uhalifu wa kiwango kikubwa cha kimataifa na yenyewe binafsi imechochea na kushiriki katika uhalifu huo.

Williams amewasilisha repoti yake leo hii kwa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa linalokutana huko Geneva.

Repoti yake imehimiza kuingilia kati kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa nguvu zaidi,uwekaji wa vikwazo na kuwashtaki wahusika wa uhalifu huo.

Repoti hiyo ya kurasa 35 imesema kwamba uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu unaendelea kutendeka katika jimbo lote la Dafur kwa kukiuka kwa makusudi haki za binaadamu na sheria ya kimataifa kwamba raia wanaendelea kuuwawa, kubakwa na kufanyiwa dhila za ngono pamoja na kuteswa.

Repoti hiyo imesema lile lililojitokeza zaidi ni kampeni ya kupambana na uasi wa Dafur kwa kutumia nguvu inayotumiwa na serikali ya Sudan kwa kushirikiana na wanamgambo wa Janjaweed na kwa kiasi kikubwa kuwalenga raia.Repoti hiyo pia inawashutumu waasi kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu na sheria ya kimataifa

Repoti inasema juhudi za kimataifa za Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na wengine kwa kiasi kikubwa zimekwamishwa na kuzuiliwa na hiyo kuthibitishwa kuwa hazitoshi na hazifai.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba takriban watu 200,000 wameuwawa huko Dafur na wengine milioni mbili na nusu wamepotezewa makaazi yao.

Mzozo huo na wimbi la wakimbizi pia umekuja kuihusisha Chad na kujenga hali ya mvutano.

Williams na timu yake wameshindwa kufanya uchunguzi katika jimbo la Dafur lenyewe kutokana na serikali ya Sudan kugoma kuwapa visa kwa kusema kwamba baadhi ya wajumbe wa timu hiyo ni watu wenye upendeleo dhidi ya Sudan madai ambayo yamerudiwa kutolewa tena hapo jana na waziri wa sheria wa Sudan wakati akiwa njiani kuelekea Geneva.

Mwezi uliopita Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu yenye makao yake huko The Hague nchini Uholanzi imewataja waziri wa serikali ya Sudan na kiongozi wa kundi la Janjaweed kuwa ni watuhumiwa wa mwanzo wanaotaka kuwashtaki kwa uhalifu wa vita juu ya mzozo wa Dafur.

Repoti juu ya hali ya Dafur inataka jumuiya ya kimataifa kuwa na msimamo kamili wa pamoja katika kulishughulikia suala la Dafur na kusaidia kuitisha mkutano wa taifa juu ya amani,haki za binaadamu na dira ya pamoja kwa Dafur.

Repoti hiyo ya Dafur inazinduwa kikao cha wiki tatu cha Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa ambalo limechukuwa nafasi ya Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa hapo mwaka 2006 ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa imepoteza sifa.

 • Tarehe 12.03.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB5J
 • Tarehe 12.03.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB5J

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com