1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yamuomboleza Kobe Bryant

27 Januari 2020

Lejendari wa mchezo wa mpira wa vikapu Kobe Bryant alifariki dunia hapo jana baada ya ndege aliyokuwa akisafiria aina ya helikopta kuanguka wakati ambapo kulikuwa na ukungu mwingi.

https://p.dw.com/p/3WsMi
USA l Ex-NBA-Superstar Kobe Bryant stirbt bei Helikopterabsturz
Picha: picture-alliance/Photoshot

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wote tisa waliokuwemo katika ndege hiyo akiwemo mwanawe wa kike.

Bryant mwenye umri wa miaka arubaini na moja alikuwa anasafiri na mwanawe Gianna aliyekuwa na umri wa miaka kumi na mitatu wakati ndege hiyo ilipoanguka katika eneo la Calabasas magharibi mwa Los Angeles. Bryant alikuwa mshindi wa Ligi ya Mchezo wa kikapu ya Marekani NBa mara tano na alishinda dhahabu ya olimpiki mara mbili.

BG Kobe Bryant | Kobe mit seiner Tochter Gianna (2019)
Kobe akiwa na mwanawe wa kike Gianna aliyefariki katika ajali hiyo piaPicha: Reuters/USA TODAY Sports/S. R. Sylvanie

Anachukuliwa na wengi kama mmoja wa wachezaji mahiri kabisa kuwahi kucheza mchezo wa mpira wa kikapu katika historia ya mchezo huo. Aliichezea timu ya Los Angeles Lakers kwa kipindi cha miongo miwili.

Del Harris ni kocha wa zamani wa LA Lakers na hapa anamzungumzia Kobe.

"Nilikuwa mkufunzi wa kwanza wa Kobe. Alikuwa na umri wa miaka 17 tu na alipotimia miaka 18 akaanza kucheza katika NBA. Alikuwa kijana mzuri sana na ameendelea hivyo hivyo kuwa mtu mzuri sana," alisema Del Harris.

Miongoni mwa waliotuma ujumbe wa kuomboleza kifo cha Bryant ni Rais Donald Trump pamoja na rais wa zamani wa Marekani Barack Obama ila kifo cha Bryant hakijawahuzunisha Wamarekani tu ila ulimwengu mzima wa michezo umejawa na majonzi.