1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yamuenzi Mandela leo

Admin.WagnerD10 Desemba 2013

Karibu viongozi 100 kutoka sehemu mbalimbali duniani wanawasili nchini Afrika Kusini Jumanne hii kuhudhuria ibada ya kihistoria, na kutoa heshima za mwisho kwa shujaa wa Afrika Kusini Nelson 'Madiba' Mandela.

https://p.dw.com/p/1AVru
Wafanyakazi wakijenga jukwaa ndani ya uwanja wa FNB ambako maelfu watamuaga Nelso Mandela.
Wafanyakazi wakijenga jukwaa ndani ya uwanja wa FNB ambako maelfu watamuaga Nelso Mandela.Picha: Getty Images

Heshima kubwa kupita kiasi kwa Nelson Mandela,mmojawapo wa vigogo vya karne ya 20,itawaleta pamoja mjini Soweto Jumanne hii, umati wa aina pekee ya viongozi wa taifa na serikali,tangu walioko madarakani mpaka waliostaafu katika tukio la kihistoria ambalo halijawahi kushuhudiwa huku zaidi ya watu 80 000 wakitarajiwa kufika katika uwanja mashuhuri wa michezo ulioko katika kitongoji hicho cha mjini Johannesburg.

Polisi wa farasi wakihakikisha usalama kabla ya kuanza kwa shughuli za kumuaga Madiba.
Polisi wa farasi wakihakikisha usalama kabla ya kuanza kwa shughuli za kumuaga Madiba.Picha: Getty Images

Maandalizi ya shughuli nzima
Heshima za mwisho na ibada rasmi inafanyika katika uwanja huo mkubwa kabisa wa dimba,kule kule zilikofanyika fainali za kombe la dunia za kabumbu mwaka 2010 na katika kitongoji kile kile cha Soweto alikoishi Nelson Mandela kabla ya kufungwa.

Kwa hivyo ni mahala pa kihistoria kumpa hishma za mwisho shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid,kwasababu eneo hilo ni kitambulisho cha kutengwa makausudi waafrika kusini weusi na wale weupe waliokuwa wakiishi Johannesburg.

"Ulimwengu mzima unafika Afrika kusini-wakiwemo viongozi mashuhuri wa dunia hii," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Afrika kusini Clayson Monyela aliyetaja majina ya viongozi kama mia moja hivi wa mataifa na serikali, wafalme au warithi wa kiti cha mfalme bila ya kuwasahau watu wengineo mashuhuri duniani ikiwa ni pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon,mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma na wanachama wa baraza la wazee aliloliunda mwenyewe Nelson Mandela.

Obama awasili Afrika Kusini
Marekani inawakilishwa na rais Barack Obama na mkewe pamoja na marais watatu wa zamani,George W. Bush,Bill Clinton na Jimmy Carter,pamoja pia na waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton, rais Raul Castro wa Cuba na Hamid Karzai wa Afghanistan wanatazamiwa pia kuhudhuria ibada hiyo rasmi ya mazishi ya Nelson Mandela sawa na waziri mkuu wa Uingereza David Camerun na mwanamfalme Charles.

Rais Pranab Mukhrejee wa India,rais Dilma Russels wa Brazil na watangulizi wake wanne ikiwa ni pamoja na Lula da Silva,waziri mkuu wa Italia Enrico Letta,kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas,waziri mkuu wa Norway,na Sweeden na mwenzao wa Canada bila ya kumsahau tukiwataja kwa uchache.

Raia wa Afrika Kusini wakisherehekea maisha ya mkombozi wao.
Raia wa Afrika Kusini wakisherehekea maisha ya mkombozi wao.Picha: Reuters

Jamhuri ya watu wa China inawakilishwa na makamo wa rais Li Yuanchao huku Japan ikiwakilishwa na mrithi wa kiti cha mfalme mwanamfalme Naruhito. Ujerumani inawakailishwa na rais wa Joachim Gauck. Viongozi kadhaa wa bara la Afrika wanahudhuria pia ibada hiyo.

Ibada hadi siku ya mazishi
Ibada kadhaa nyengine zinafanyika hadi siku ya mazishi ya Mandela katika kijiji wazee wake walikotokea huko Qunu,Desemba 15 ijayo.Mbali na ibada rasmi ya mazishi hii leo,maiti ya Nelson Mandela itawekwa katika ikulu kuanzia jumatano hadi ijumaa itakaposafirishwa kwa ndege hadi Mashariki ya Cape town kwa mazishi.

Hatua za ulinzi zimeimarishwa.Afrika kusini inauzoefu kutokana na maandalizi ya kombe la dunia la dimba mwaka 2010."Kila kitu tayari,tumejiandaa tangu miaka mitatu au minne iliyopita-waziri wa ulinzi Nosiviwe Mapisa-Nqakula amesema.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,dpa/AFP
Mhariri. Mohammed Abdul-rahman