1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yakumbuka maangamizi ya Wayahudi

Abdu Mtullya27 Januari 2016

Watu duniani kote wanaadhimisha mwaka wa 71 tangu kukombolewa kwa kambi ya maangamizi ya Auschwitz nchini Poland. Ni katika kambi hiyo ambamo mafashisti wa Kijerumani waliwaangamiza Wayahudi.

https://p.dw.com/p/1HkYF
Polen Ausschwitz Gefangene 70 Jahre Befreiung
Picha: picture-alliance/dpa/V. Melnikov

Katika kuwakumbuka wayahudi na watu wengine waliongamizwa na mafashisti katika kambi Auschwitz, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesisitiza umuhimu wa kupambana na aina zote za ubaguzi.

Steinmeier amesema ikiwa wayahudi na watu wengine wenye maoni tofauti, barani Ulaya kote, hawatahisi kuwa salama, basi hapatakuwapo tena mtu yeyote ataehisi kuwa salama.

Steinmeier amekumbusha juu ya wayahudi Milioni sita na watu wengine waliouliwa na mafashisti. Amesema watu wote, na siyo viongozi tu, wanao wajibu wa kuutimiza katika kupinga aina zote za ubaguzi.

Bunge la Ujerumani Jumatano limeadhimisha mwaka wa 71 tangu kukombolewa kwa kambi ya maangamizi ya Auschwitz na majeshi ya Umoja wa Kisoviet. Maadhimisho hayo yamefanywa kwa maonyesho yaliyofunguliwa na Spika wa Bunge Nobert Lammert.

Mgeni wa heshima amekuwa mtaalamu Ruth Klüger alieotoa hotuba. Mtaalamu huyo ni miongoni mwa watu wachache walionusurika maangamizi kwenye kambi ya Auschwitz nchini Poland.

Kansela Merkel ahimiza mafunzo ya historia kwa vijana

Ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha ukombozi huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mapema wiki hii alifungua maonyesho ya kazi za sanaa za watu waliofungwa kwenye kambi hiyo. Kansela Merkel amesema maonyesho hayo yanapaswa kuwa mafunzo muhimu ya historia kwa vijana.

Kansela Angela Merkel na Ernst Cramer alienusurika maangamizi
Kansela Angela Merkel na Ernst Cramer alienusurika maangamiziPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Amesema mafunzo hayo ni muhimu hasa wakati huu ambapo Ujerumani inapokea idadi kubwa ya wakimbizi hasa kutoka Mashariki ya Kati. Kiongozi huyo wa Ujerumani amesema mkazo unapaswa kuwekwa hasa juu ya vijana wanaotoka katika nchi ambako chuki dhidi ya Wayahudi imeenea.

Katika kuwakumbuka watu walioangamizwa na mafashisti kwenye kambi ya Auschwitz, Rais Obama leo atawaenzi watu wanne ikiwa pamoja na Wamarekani kutoka majimbo ya Indiana na Tennessee waliohatarisha maisha yao ili kuwalinda wayahudi .

Rais Obama ameungana na viongozi wa wayahudi kwenye ubalozi wa Israel mjini Washington ili kuwakumbuka mamilioni ya watu waliongamizwa na mafashisti. Watu zaidi ya 1,300,000 waliangamizwa na mafashisti kwenye kambi ya Auschwitz kabla ya kukombolewa na majeshi ya Umoja wa Kisoviet.