1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yawaachia huru wanaharakati wa Demokrasia

Admin.WagnerD26 Desemba 2018

Wanaharakati wanne wa vuguvugu la Filimbi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo wameachiwa huru baada ya mwaka mmoja jela na siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu uliocheleweshwa kwa muda mrefu. 

https://p.dw.com/p/3AeHR
Ein Mitglied von Lucha demonstriert in Goma
Picha: D.Kannah/AFP/Getty Images

Vyombo vya habari nchini jamhuri ya kidemokrasi ya congo vimenukuu duru za kuaminika zikisema wanaharakati hao waliachiwa jana jumanne kutoka gereza la Makal mjini Kinshasa.

Kituo cha radio cha Okapi kinachosimamiwa na umoja wa mataifa kimeripoti kuwa wanaharakati walioachiwa huru ni pamoja mratibu wa vuguvugu la Filimbi Carbone Beni na wanachama wengine watatu ambapo walikamatwa na kuwekwa korokoroni mwaka uliopita.

Wanaharakati hao walikamatwa mwezi Disemba mwaka jana baada ya kuitisha maandamano makubwa ya umma kumpinga rais Joseph Kabila.

Mwezi Septemba walihukumiwa kwenda jela kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kutenda kosa dhidi ya mkuu wa nchi miongoni mwa mashtaka mengineyo.

Kabla ya hukumu hiyo wanaharakati hao walikuwa wamezuiliwa katika eneo la siri kwa miezi kadhaa.

Vuguvugu lingine la kupigania mabadiliko la Lucha limesifu kuachiwa huru kwa wanaharati hao na kuiita hukumu dhidi yao kuwa isiyo ya haki na kwamba iliamriwa na rais Joseph Kabila.

Wasiwasi juu ya mashine za kupigia kura waendelea

Demokratische Republik Kongo Wahlmaschine
Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Katika hatua nyingine, hapo jana wagombea kadhaa wa upinzani waliyatolea wito makampuni yote ya simu nchini DRC kuzizima kadi za simu zinazotumika kwenye mashine za kupigia kura wakiamini zinaweza kuwaruhsuu maafisa wa serikali kuhamisha matokeo ya kura kutoka kwenye mashine hizo kabla ya kuhesabiwa.

Wagombea saba wa upinzani akiwemo Martin Fayulu wamesema wana wasiwasi kuwa tume ya uchaguzi inaweza kuhamisha na kujumlisha matokeo kwa njia ya kielectroniki jambo ambalo ni kinyume na uamuzi wa pamoja unaotaka kura zihesabiwe kwa njia ya kawaida baada ya kuchapishwa kutoka kwenye mashine hizo.

Kuhusu hilo mgombea wa urais Ngoy Ilunga Nsenga kutoka chama cha haki nchini DRC amesema

"Tunawaomba watoa huduma wote wa simu waliopo DC, Vodacom, orange na wengineo kuwapatia wakongomani namba zote za simu za kadi walizowauzia tume ya uchaguzi CENI; na tunawarai kuwa wazizime ili kutii sheria za uchaguzi.”

Wapinzani wamekuwa wakilalamikia uamuzi wa kutumia mashine za kielektroniki ambazo wanahofia zinaweza kutumika kufanya udanganyifu kwenye matokeo.

CENI imetetea matumizi yake

Demokratische Republik Kongo Wahlmaschine
Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Maafisa wa tume ya uchaguzi wametetea mara kadhaa uamuzi wa kutumia mashine za elektroniki wakisema zitaufanya uchaguzi huo kuwa wenye ufanisi.

Uchaguzi wa rais, bunge na majimbo nchini DRC ulikuwa ufanyike Jumapili iliyopita kumaliza vuta nikuvute ya kiasi miaka miwili juu ya hatma ya rais Kabila

Hata hivyo tume ya uchaguzi nchini humo ilitangaza kuhairisha uchaguzi huo kwa kipindi cha wiki moja kutokana na vifaa vya kupigia kura ikiwemo mashine za kielektroniki kuteketea kwa moto kwenye ghala la vifaa hivyo mjini Kinshasa.

Mwandishi Rashid Chilumba/AFP/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo