DRC kuathirika na njaa iwapo ufadhili utakatizwa | Matukio ya Afrika | DW | 18.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

DRC kuathirika na njaa iwapo ufadhili utakatizwa

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa takriban watu milioni 13 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watakabiliwa na kitisho cha njaa iwapo misaada ya kifedha itaendelea kupungua. Jamii ya kimataifa yaombwa isaidie.

Umoja wa Mataifa ulitoa tahadhari hapo jana kwamba janga la kibinadamu linaweza kutokea katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya miaka mitatu ya kuendelea kupungua kwa ufadhili wa kuwezesha upatikanaji wa chakula ambao ulifikia kwenye kiwango kibaya mwaka jana wa 2017 hasa katika jimbo la Kasai linalokabiliwa na migogoro. 

Jean-Philippe Chauzy msemaji wa shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM)

Jean-Philippe Chauzy msemaji wa shirika la kimataifa la uhamijai IOM

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji anayeshughulikia Kongo Jean-Philippe Chauzy amesema watoto ndio wanaoathirika zaidi katika jimbo hilo na kwamba wanaweza kufa iwapo misaada ya kifedha itakatizwa. Shirika hilo ia IOM limesema limetoa ombi la kiasi cha dola milioni 75 ili kuisaidia Kongo ambapo kufikia sasa wamepokea   kiasi cha dola milioni 3.5 pekee.

Nembo ya shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM)

Nembo ya shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM)

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM limesema jumla ya watu milioni 13.1 watahitaji msaada nchini Kongo katika mwaka huu wa 2018 idadi hiyo ikiwa imeongezeka kwa asilimia 80 ikilinganishwa na mwanzoni mwa mwaka uliopita. Watu milioni 7.7 wamo katika hali mbaya zaidi na wanahitaji misaada ya chakula kwa haraka.

Mnamo mwaka wa 2017 mgogoro mkubwa uliojawa na matendo ya kikatili ulilikumba jimbo la Kasai lililopo kusini magharibi mwa Kongo. Mgogoro huo ulisababisha jamii ya kimataifa kuelekeza lawama kwa wapiganaji wanaoiunga mkono serikali kwa kuhusika na mauaji ya raia lakini wakati huo huo kuongezeka kwa vurugu kutoka kwa makundi ya waasi katika mikoa ya mashariki  inayopakana na nchi za Uganda, Rwanda, Tanzania, Burundi na Zambia hakukutiliwa maanani sana.

Kwa mujibu wa bwana Jean- Philippe Chauzy, wapiganaji wa makundi ya waasi katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanashirikiana kumpinga Rais Joseph Kabila.

Mwandishi Zainab Aziz/RTRE

Mhariri: Gakuba Daniel