DR Congo: Maalfu wakimbia kwenda nchi jirani ya Rwanda | Matukio ya Afrika | DW | 23.05.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Goma

DR Congo: Maalfu wakimbia kwenda nchi jirani ya Rwanda

Watu wapatao 3,000 wameukimbia mji wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Goma kuelekea Rwanda leo Jumapili baada ya mlipuko wa volcano katika mlima Nyiragongo.

Balozi wa Rwanda nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Vincent Karega ameandika kwenye Twitter kwamba "mipaka iko wazi na majirani zetu wanakaribishwa kwa amani".

Serikali nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeagiza watu waondolewe kutoka mji wa mashariki wa Goma, baada ya kutokea mlipuko huo wa volcano katika mlima Nyiragongo uliopo karibu na mji huo wa mpakani.

Afisa mmoja katika hifadhi ya kitaifa ya Virunga iliyopo kwenye eneo ambako volcano imelipuka amesema hadi hii leo asubuhi tope la moto linalotiririka kutoka kwenye mlima Nyiragongo limefika kwenye uwanja wa ndege wa mji huo wa Goma na kwamba hali inazidi kuwa mbaya.

Afisa huyo amesema anahofia kwamba tope hilo la moto (Lava) linaweza kufika hadi kwenye fukwe za ziwa Kivu. Amesema mlipuko huo unalingana na ule uliotokea mwaka 2002 na amewataka raia waondoke mahala hapo haraka.

Baadhi ya raia wa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaoondoka mjini Goma kukimbia mlipuko wa volcano kwenye mlima Nyiragongo.

Baadhi ya raia wa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaoondoka mjini Goma kukimbia mlipuko wa volcano kwenye mlima Nyiragongo.

Waziri wa mawasiliano Patrick Muyaya aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba hatua za kuwahamisha zimeanza kutekelezwa.

Hata hivyo kabla ya serikali kutoa agizo hilo, maalfu ya raia walikuwa tayari wameshaanza kukimbia. Huduma ya umeme ilikatika kwenye maeneo mengi kabla ya mamia ya wakaazi wa mji huo kuanza kuondoka. Baadhi yao walielekea kusini karibu na mpaka kati ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.

Wengine walielekea magharibi kwenye mji wa Sake uliopo kwenye jimbo la Masisi la nchi jirani ya Jamuhuri ya Congo. 

Kushoto: Rais wa Rwanda Paul Kagame. Kulia: Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi.

Kushoto: Rais wa Rwanda Paul Kagame. Kulia: Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi.

Volcano ilianza kulipuka kwenye mlima Nyiragongo kuanzia saa moja usiku Jumamosi, moshi mzito mwekundu ulionekana angani.

Gavana wa jeshi katika jimbo la Kivu Kaskazini, Jenerali Constant Ndima amewataka wananchi kuwa watulivu na wakati huohuo wafuate maelekezo yanayotolewa na maafisa wa serikali. Gavana Ndima aliyasema hayo kupitia kwenye radio ya mji huo.

Katika ripoti yao ya Mei 10, wataalamu wa Goma walitoa tahadhari juu ya kuongezeka ishara za kulipuka kwa volkano na walipendekeza kuzifuatilia ishara hizo kwa makini. Mnamo siku ya Jumamosi kituo cha wataalamu hao kilitoa taarifa kwamba mtiririko wa lava, ulikuwa unaelekea katika nchi jirani ya Rwanda.

Katika mlipuko wa volcano uliotokea Januari 17, mwaka 2002, watu zaidi ya 100 walikufa. Mlipuko mbaya zaidi wa volkano uliofikia hadi mita 3,000 kwenda juu ulitokea mnamo mwaka 1977. Watu zaidi ya 600 walikufa.

Eneo la Goma, liko katika mkoa wa Kivu Kaskazini mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na linapakana na nchi za jirani za Rwanda na Uganda.

Chanzo:/AFP