1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund kuchuana na Leipzig DFB Pokal

3 Mei 2021

Hata bila ya Erling Haaland kuwa kikosini Borussia Dortmund walifunga magoli mengi katika mchuano wao wa nusu fainali ya DFB Pokal. Miamba hao waliwazaba Holstein Kiel 5-0.

https://p.dw.com/p/3suTf
DFB Pokal | Halbfinale | BVB vs Holstein Kiel | Tor (3:0)
Picha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Giovanni Reyna akipachika wavuni mabao mawili, Marco Reus, Thorgan Hazard na Jude Bellingham wakiwa wachezaji wengine waliocheka na wavu katika mechi hiyo.

Ushindi huo sasa umewahakikishia Dortmund nafasi ya fainali ambapo watakuwa wanakwaana na mahasimu wao katika ligi RB Lepzig ambao kwenye mechi yao ya nusu fainali waliwalaza Werder Bremen 2-1 baada ya Emil Frosberg kufunga goli katika dakika ya mwisho ya muda wa ziada.

DFB Cup - Semi Final - Werder Bremen vs. RB Leipzig
Kiungo wa RB Leipzig Emil ForsbergPicha: Cathrin Mueller/AFP

Lakini hata kabla ya fainali hiyo, Dortmund watakuwa wanawaalika Lepzig kwenye mechi ya Bundesliga Jumamosi hii inayokuja wakati ambapo BVB wanatafuta nafasi ya kushiriki Champions League msimu ujao.

Ni mechi tatu tu zilizosalia msimu wa Bundesliga kufikia mwisho na kwa sasa Dortmund wanaishikilia nafasi ya tano wakiwa na pointi 55 na timu iliyo juu yao Eintracht Frankfurt ikiwa na pointi 56, huku timu inayoishikilia nafasi ya tatu VfL Wolfsburg ikiwa na pointi 57.

Kwa hiyo ushindi wa Dortmund watakapocheza na Leipzig wenye pointi 64 katika nafasi ya pili na iwapo Wolfsburg na Frankfurt watapoteza mechi zao, basi utawapelekea kuingia kwenye timu tatu bora.