Diplomasia ndiyo itafanikiwa Mashariki ya Kati | Magazetini | DW | 11.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Diplomasia ndiyo itafanikiwa Mashariki ya Kati

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya hali ya Mashariki ya Kati, mkasa mwingine wa ujasusi unaofanywa na Marekani nchini Ujerumani na pia wanatoa maoni juu ya Kombe la Dunia.

Mgogoro wa Mashariki ya Kati

Mgogoro wa Mashariki ya Kati

Mhariri wa gazeti la Rhein-Necker anasema mashambulio ya makombora, utekaji nyara na mauaji ni upande mmoja tu katika mgogoro wa Mashariki ya Kati. Hata hivyo, anasema mambo hayo yanachochea chuki.

Mhariri huyo anaamini kwamba kinachotakiwa sasa katika Mashariki ya Kati ni juhudi za kidiplomasia, akihoji kwamba wakati umefika kwa Umoja wa Mataifa kulichukua jukumu la mazungumzo juu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati kwa lengo la kupatikana nchi ya Wapalestina.

Mazungumzo yameshindikana

Gazeti la Pforzheimer linasema damu inayomwagika sasa katika Mashariki ya Kati ni dalili ya kushindwa kusonga mbele kwa mazungumzo baina ya Israel na Wapalestina. Hamas imekwama na serikali ya Israel imepoteza dira. Lakini pande zote zinajua kwamba matumizi ya silaha siyo suluhisho.

Mawazo kama hayo anayo mhariri wa gazeti la Der Neue Tag amabye naye anasisitiza umuhimu wa kupatikana suluhisho katika Mashariki ya Kati, kwa kusema kwamba idadi ya watu wasiokuwa na hatia, wanaoathirika na mapigano katika Mashariki ya Kati, inazidi kuongezeka. Hali hiyo inatokana na kushindikana kwa mazungumzo juu ya kulifikia suluhisho la kuundwa nchi ya Wapalestina. Lakini hakuna njia nyingine.

Sakata la ujasusi


Mkasa mwingine wa ujasusi unaofanywa nchini Ujerumani na Marekani umebainika. Wajerumani wanasema sasa Marekani inavuka mipaka

Gazeti la Lausitzer Rundschau linaeleza kwamba ujasusi unafanyika kwenye wizara ya ulinzi na kwenye Bunge na pia simu ya Kansela Angela Merkel na zile za viongozi wengine zinadukuliwa. Hatua hizo zinavuka mipaka na pia ni vitendo vya kihalifu.

Gazeti la Nürnberger Nachrichten linataka hatua zichukuliwe na linashauri kwamba kwenye mazungumzo juu ya kuuanzisha ukanda huru wa biashara baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani, lazima suala la kulinda siri za nchi lizingatiwe. Ni wazi kwamba Marekani ingekasirika sana iwapo Edward Snowden aliyefichua siri za mashirika ya ujasusi ya Marekani angelialikwa kuja Ujerumani, lakini kwa upande mwingine Marekani inastahili kufanyiwa hilo.

Ujerumani na Kombe la Dunia

Gazeti la Westdeutsche linasema timu ya Ujerumani ndiyo yenye matumaini makubwa ya kulibeba kombe. Sababu ni kwamba inayo tajiriba ya mashindano yaliyopita. Mnamo mwaka wa 2006 iliishia katika nusu fainali, na mnamo mwaka wa 2010 pia ilikwamia katika nusu fainali. Pia katika Kombe la Ulaya, mnamo mwaka wa 2008, Ujerumani ilitolewa katika fainali. Timu ya Ujerumani imejifunza kutokana na tajiriba hizo na bado hatua moja tu safari hii kulifikia lengo.

Vyanzo: Westdeutsche, Nürnberger Nachrichten, Lausitzer Rundschau, Der Neue Tag, Pforzheimer, Rhein-Necker
Mhariri: Yusuf Saumu