Diack: riadha inakabiliwa na mgogoro | Michezo | DW | 22.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Diack: riadha inakabiliwa na mgogoro

Rais anayeondoka wa shirikisho la kimataifa la riadha – IAAF lamine Diack amekiri kuwa mchezo huo upo katika mgogoro kwa sababu ya madai ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini yaliyotolewa dhidi ya shirikisho

IAAF imekabiliwa na wiki tatu ngumu kabisa za ufichuzi wa fedheha na madai kuwa imezembea na kupuuza jukumu lake la kuangamiza udanganyifu wa dawa zilizopigwa marufuku. "Tuamini. Hatuwezi kuwapa nafasi watu kuwa na mashaka na kazi zetu, tukifanya hivyo tutakuwa tumekwisha. Ikiwa kuna masuala kuhusu tunachokifanya basi tumekwisha lakini tuna uhakika kuwa asilimia 99 ya wanariadha wetu ni wasafi. Tunaendelea kufanya kazi yetu kama tu tunavyofanya tu kila mara. Siyo kwamba mengi yanayosemwa kuhusu suala la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini yatatupa hofu. Tutaendelea na kazi ile ile kwa sababu hakuna kipya cha kujifunza".

Miaka 16 ya Diack kama rais wa IAAF inakamilika wakati nafasi yake itakapochukuliwa na rais mtarajiwa Sebastian Coe baada ya kukamilika mashindano ya ulimwengu ya riadha mjini Beijing. Diack, raia wa Senegal anasema ana matumaini kuwa mrithi wake Coe, ambaye tayari ametangaza kuwa ataunda shirika huru la kupambana na dawa za kuongeza nguvu mwilini katika riadha, ataweza kutekeleza jukumu la kuulinda mchezo huyo dhidi ya wakosoaje wake.

Großbritannien Sebastian Coe Präsident des Leichtathletik-Weltverbandes IAAF

Rais mpya wa IAAF Sebastian Coe

Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC Thomas Bach ambaye amehudhuria sherehe za ufunguzi wa mashindano ya dunia ya riadha mjini Beijing amesema kuwa IOC itashirikiana kwa karibu na Coe na shirikisho lake katika vita dhidi ya dawa zilizopigwa marufuku."Tutafanya kazi kwa pamoja katika utekelezaji wa sera ya kupambana na dawa zilizopigwa marufuku na tutafanya kila tuwezalo katika mamlaka yetu kuwalinda wariadha wasafi. Wakati tukiwalinda wanariadha wasafi katika hali hii pia ina maana kuwa hatutoi madai dhidi ya wanariadha ambao hawana hatia hadi pale itakapothibitishwa".

Bolt ahuzinishwa

Na wakati hayo yakijiri, bingwa wa Olimpiki na Dunia wa mbio za masafa mafupi Usain Bolt amesema kuwa amehuzunishwa na namna mchezo wa riadha ulivyochafuliwa na ripoti za matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini. Bolt anasema inahuzunisha kuwa habari za udanganyifu katika riadha ndizo zilizotawala katika vyombo vya habari kabla ya kuanza mashindano ya ubingwa wa Ulimwengu mjini Beijing, na wala sio ushindani unaotarajiwa kushuhudiwa. "Suala la dawa za kuongeza nguvu mwilini limetawala vichwa vya habari katika miezi kadhaa iliyopita. Inahuzunisha kuwa hapo ndipo mchezo huu umefikia sasa. kuna matumaini kuwa rais mpya wa IAAF anaweza kufanya marekebisho makubwa ya sheria na kufanya mambo yawe rahisi kwa mchezo huu kuwa bora. Hivyo tutaona kitakachotokea".

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Mohamed Dahman