1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Diack ajiuzulu kama mwanachama wa IOC

12 Novemba 2015

Rais wa zamani wa Shirikisho la Riadha la Kimataifa - IAAF Lamine Diack amejiuzulu kama mwanachama wa heshima wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki - IOC

https://p.dw.com/p/1H4Qf
Lamine Diack IAAF Präsident PK
Picha: Getty Images/C. Hawkins

Diack alikuwa tayari amesimamishwa kwa muda na IOC wakati akiendelea kuchunguzwa na maafisa wa polisi wa Ufaransa kwa tuhuma za kupokea hongo ili kuficha wanariadha waliogunduliwa wametumia dawa haramu alipokuwa uongozini IAAF.

Msenegal huyo mwenye umri wa miaka 82, ambaye ameiongoza IAAF kwa miaka 16 tayari amejiuzulu kutoka kwa wakfu wa IAAF, unaosimamiwa na IAAF.

IAAF imetumbukia katika mgogoro kuhusu tuhuma za matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini kufuatia ripoti iliyotolewa na shirika la kimataifa la kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli - WADA.

Mwanawe Diack, Papa Massata Diack, mshauri wake Habib Cisse na mkuu wa zamani wa kukabiliana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini katika IAAF Gabriel Dolle pia wanachunguzwa na maafisa wa polisi wa Ufaransa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman