1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Diab aomba wafadhili kuiokoa lebanon inayokumbwa na migogoro

Zainab Aziz
6 Julai 2021

Waziri mkuu wa kipindi cha mpito Hassan Diab amesema Lebanon inakaribia kusambaratika kijamii na ameziomba nchi rafiki na taasisi za kimataifa ziisaidie katika juhudi zake za kukabiliana na matatizo makubwa ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/3w7Cs
Libanon Beirut | Rede zur Wirtschaftskrise | Hassan Diab
Picha: Lebanese Gov't Press Office/Anadolu Agency/picture alliance

Waziri Mkuu Hassan Diab amesema Lebanon inapitia katika njia ya gizani na shida zake zimefikia kiwango cha maafa. Ameeleza kwamba shida hizo zilizoikumba kila sekta ya jamii zinailekeza Lebanon kwenye dimbwi refu la matatizo.

Serikali ya waziri mkuu wa mpito Hassan Diab iliojiuzulu baada ya kutokea mlipuko kwenye bandari ya Beirut mnamo mwezi agosti imetoa wito wa kuundwa serikali mpya haraka ili kuweza kuushughulikia mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaoizorotesha Lebanon. Benki ya dunia imesema Lebanon inapitia kipindi kirefu cha mgogoro wa kiuchumi ambao ni miongoni mwa migogoro mikubwa duniani tangu miaka ya 1800.

Hasira ya watu juu ya uhaba wa mafuta imesababisha vurugu na mapigano katika vituo vya kuuzia mafuta jambo ambalo linamfanya waziri mkuu wa mpito wa Lebanon Hassa Diab atoe tahadhari kwamba anahofia yatatokea machafuko zaidi nchini humo.

"Kuundwa kwa serikali mpya kumecheleweshwa kwa muda mrefu na Walebanon kwa muda mrefu wamebeba mzigo wa kusuburi lakini uvumilivu wao umeanza kumalizika huku shida na mateso yakizidi kuongezeka. Kujuimuisha pamoja wazo la kutafuta msaada kwa ajili ya Walebanon na uundwaji wa serikali mpya limekuwa ni tishio kwa maisha ya Walebanon na mustakabali wa Lebanon,” alisema Diab

Israel yajitolea kuisadia Lebanon

Israel Verteidigungsminister Benny Gantz
Waziri wa ulinzi wa Israel Benny GantzPicha: Abir Sultan/Pool Photo via AP/picture alliance

Mivutano ya ndani na kutokuwapo serikali tangu mwezi wa Oktoba ni mambo yanayochangia katika kuchelewesha kuyashughulikia matatizo yanayoikabili Lebanon. Thamani ya sarafu ya nchi hiyo Pauni ya Lebanon, imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 90 tangu mwaka 2019.

Waziri wa ulinzi wa Israel Benny Gantz, amesema nchi yake inajitolea kupeleka misaada kwa Lebanon kupitia Umoja wa Mataifa. Hata hivyo Lebanon na Israel kimsingi ni nchi zilizomo vitani na pana mivutano ya mara kwa mara kwenye mpaka baina yao kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran.

Waziri mkuu huyo wa Lebanon wa kipindi cha mpito Hassan Diab alikutana na mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali mjini Beirut. Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell wiki jana aliwalaumu viongozi wa Lebanon kwa kusababisha migogoro hiyo ya kiuchumi na kisiasa. amesema ni serikali mpya tu itakayoweza kuazisha tena mazungumzo na shirika la fedha la kimataifa IMF juu ya kuutatua
mgogoro wa kiuchumi wa Lebanon. Ameeleza kuwa serikali ya sasa haina haki ya kufanya mazungumzo hayo juu ya kuutekeleza mpango wa kuufufua uchumi kwa sababu amesema mpango huo unaweza kuwa na vipengele ambavyo havitakubalika na serikali ijayo. 

Waziri mkuu wa mpito hassan Diab ametaka miito juu ya kutoa misaada iambatanishwe na mageuzi. Ameeleza kuwa vikwazo vilivyowekwa haviwagusi mafisadi ambao ni baadhi ya viongozi.

Licha ya shinikizo la kimataifa, ambapo Ufaransa mkoloni ya zamani wa Lebanon kuongoza shinikzo hilo, wanasiasa waliokita mizizi ambao wamegawanyika wameshindwa kukubaliana juu ya kuchagua safu itakayounda baraza la mawaziri kwa karibu miezi 11.

Vyanzo:/DPA/AFP