1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dhana za Rwanda dhidi ya Ufaransa

Hamidou, Oumilkher7 Agosti 2008

Serikali ya mjini Paris yahoji ripoti ya kamisheni ya uchunguzi ya Kigali ni ya mapendeleo

https://p.dw.com/p/EsEX
Mabufuru ya wahanga wa mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994Picha: AP



Ufaransa inakanusha madai ya kuhusika na mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda na kuitaja ripoti ya kamisheni ya uchunguzi ya serikali ya Kigali kua "si ya kukubalika",ikisisitiza hata hivyo azma ya kupalilia uhusiano wa kibalozi ulioanza kuchipuka upya tangu mwaka mmoja uliopita.


"Ripoti ina tuhuma zisizokubalika dhidi ya viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Ufaransa"-amesema hayo msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje  Romain Nadal wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari mjini Paris.


Ripoti ya kamisheni ya uchunguzi kuhusu mauwaji ya halaiki,iliyochapishwa jumanne iliyopita mjini Kigali,inaituhumu Ufaransa "kua iliarifiwa juu ya maandalizi ",na kushiriki mipango ilipokua ikiandaliwa na katika kuitekeleza pia."



Japo kama tuhuma hizo dhidi ya Ufaransa si mpya,hata hivyo ripoti hiyo inazungumzia kwa mara ya kwanza uwezekano wa kuandamwa kisheria viongozi wa zamani wa kisiasa na kijeshi wa Ufaransa.


Ripoti hiyo inawalaumu miongoni mwa wengineo,rais wa zamani wa Ufaransa Francois Mitterrand,waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje Alain Juppé na kuwatuhumu wanajeshi wa Ufaransa kushiriki katika mauwaji na ubakaji.


Waziri wa sheria wa Rwanda Tharcisse KARAGURAMA anasema:



"Inaonyesha jinsi Ufaransa iliovyochangia katika mauwaji ya halaiki.Inaonyesha pia mchango wa Ufaransa baada ya mauwaji ya halaiki kwa kuwalinda waliofanya mauwaji hayo na kukorofisha juhudi za kuwakamata na kuwafikisha mahakamani."


Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa inaiwekea suala la kuuliza kamisheni ya uchunguzi ya Rwanda iliyoundwa mwaka 2006 ,huku wizara ya ulinzi ya mjini Paris ikidai kamisheni hiyo "haijatakasika na dhana za mapendeleo".


Jeshi la Ufaransa linang'ang'ania msimamo ule ule likihoji Ufaransa imetekeleza kikamilifu wajib wake  nchini Rwanda mnamo mwaka 1994,ikiwa ni pamoja na kusimamia opereshini ya kijeshi na kiutu iliyokua ikijulikana kama "opereshini ya Feruzi."


Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje Alain Juppé amelaumu kile alichokiita "kupotosha  makusudi ukweli wa mambo."


Shirika la Ufaransa kwa jina Survie linasema Ufaransa haistahiki kupuuza yaliyoandikwa ndani ya ripoti hiyo.Shirika hilo limetoa mwito ukweli utamkwe.


Nchini Rwanda pia shirika linalotetea masilahi ya walionusurika-kwa jina IBUKA,ikimaanisha kwa  kinyarwanda-Kumbuka, limeitolea mwito Ufaransa iwafungulie mashtaka watuhumiwa waliotajwa ndani ya ripoti hiyo.


"Vyombo vya sheria vya Ufaransa vinabidi viwe vya mwanzo kuwaandama watuhumiwa na kuhakikisha wahanga wanalipwa fidia" amesema hayo mwenyekiti wa shirika la Ibuka Theodore Simburudari.