Deutsche Welle: Makala ya Afrika Wiki hii | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.02.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Deutsche Welle: Makala ya Afrika Wiki hii

Karibu katika makala nyengine ya Afrika wiki hii, Uchambuzi wa baadhi ya yale muhimu yaliotokea Afrika mnamo juma hili.

default

Miongoni mwayo ni hali ya kisiasa nchini Kenya, kukizuka mvutano mwengine kati ya pande mbili zinazounda serikali ya Muungano nchini humo -kikao cha halmashauri kuu ya chama tawala nchini Tanzania CCM chamalizika , kikitoa sura ya mustakbali wake Ivory Coast nayo yaingia katika mgogoro mwengine wa kisiasa na rais Robert Mugabe wa Zimbabwe atoa wito vikwazo dhidi ya nchi yake viondolewe.

Lakini kwanza tunaanzia na kile kilichogonga vichwa vya habari Juma hili, ambacho ni mapinduzi ya kijeshi nchini Niger dhidi ya rais

Mamadou Tandja, ambaye mwaka jana alizusha hali ya wasi wasi kutokana na majaribio yake ya kung'ang'ania madaraka, alipoibadili katiba na kuitsha kubadili kifungu cha mihula miwili ya uongozi.

Präsident der Republik Niger, Mamadou Tandja

Rais Mamadou Tandja

Wanajeshi walioasi waliivamia Ikulu ambako rais huyo alikuwa na mkutano na baraza la mawaziri. Kulizuka milio ya risasi na moshi ukionekana kufuka katika jengo hilo la Ikulu. Kulikuwa na hali ya mtafaruku kwa muda wa masaa kadhaa, kabla ya Kanali Goukoye Abdul Karimou kujitokeza kwenye televisheni na kuliarifu taifa kwamba rais Tandja amepinduliwa. Alisema Baraza kuu kwa ajili ya kurejesha demokrasi nchini Niger limeisimamisha katiba na kuzivunja taasisi zote.

Taarifa ya Kanali huyo kama msemaji wa baraza hilo ilitolewa akiwa amezungukwa na wanajeshi wenzake. Rais Tandja alikuwa akizuiliwa katika kambi moja ya kijeshi mjini Niamey.

Jumuiya ya uchumi ya Afrika magharibi ECOWAS, iliisimamisha uanachama Niger baada ya Tandja kuibadili katiba na kujiongezea muda wa madaraka kwa kuitisha uchaguzi uliosusiwa na vyama vya upinzani. Marekani na Umoja wa Ulaya pia vikaiwekea vikwazo nchi hiyo. Taarifa ya Marekani baada ya mapinduzi hayo ya Alhamisi ilisema wakati inalaani utwaaji madaraka kwa nguvu, ina matumaini kwamba Niger itarejea haraka katika utawala wa kidemokrasi.

Katika eneo la Mashariki mwa bara hilo la Afrika, huko nchini Kenya pande mbili zinazounda serikali ya muungano nchini Kenya zimeingia katika mgogoro mpya wiki hii, baada ya Jumapili iliopita, Waziri mkuu Raila Odinga kuwasimamisha kazi mawaziri wawili , William Ruto waziri wa kilimo na mwenzake wa elimu Sam Ongeri hadi utakapomalizika uchunguzi juu ya shutuma za rushwa zinazowakabili. Lakini muda mfupi baadae Rais Mwai Kibaki akasema hatua hiyo si halali kwa msingi wa kwamba Bw Odinga hana mamlaka hayo,pamoja na kwamba Waziri mkuu huyo anasema ni yeye anayeongoza shughuli za serikali.

Kutokana na mvutano huo ambao umetaoa sura paia ya kuwepo kwa mgawanyiko ndani ya chama cha ODM cha Bw Raila ambacho

Kenia Bekanntgabe des Kabinetts Odinga hinter Kibaki

Rais Kibaki na Raila Odinga

Bw Ruto ni miongoni mwa vigogo wa chama hicho, ODM ikasema itasusia vikao vyote vya baraza la mawaziri.

Wakati Mudavadi akitangaza hayo, mbunge wa Mombasa na Waziri wa utalii ambaye pia ni mwanachama wa ngazi ya juu katika ODM Bw Najib Balala akizungumzia kadhia hiyo alisema:-

Ama katika kile kilichoonekana kuwa ni kujibu kitisho cha ODM, chama cha PNU mshirika katika serikali ya mseto, kikatoa taarifa yake mjini Nairobi. Mwandishi wetu mjini humo Alfred Kiti alituarifu zaidi.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa barani Afrika , wameonya kuhusu uwezekano wa mvutano huo kati ya ODM na PNU kuwa mkubwa zaidi na hatari ya kuzuka tena machafuko pindi ukipamba moto. Waziri mkuu Raila Odinga kwa upande amemuomba Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa Koffi Annan aliyekuwa mpatanishi wa mgogoro uliozuka baada ya uchaguzi 2007 na kusababisha pande hizo hatimae kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya muungano, aingilie kati mvutano huu mpya akisema rais Kibaki anaweka vikwazo vya kutekelezwa makubaliano yaliofikiwa.

Pamoja na hayo kulipatikana taarifa siku ya Alhamisi kwamba viongozi wa ODM na PNU watakutana Jumapili hii kutafuta suluhisho la mgogoro huo. Akithibitisha hayo katika mahojiano na DW, Katibu mkuu wa ODM Profesa Peter Anyang Nyo´ngo alisema.

Katika nchi jirani na Kenya-Tanzania, chama tawala CCM kilimaliza kikao chake cha halmashauri kuu ya taifa mjini Dodoma kilichoitishwa kuzungumzia masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na mvutano kati ya makundi mawili chamani huku moja likisema linapigana dhidi ya ufisadi, na pia hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, kufuatia makubaliano ya kuondoa uhasama kati ya CCM Zanzibar na chama cha upinzani CUF, kukiwa na uwezekano hatimae wa kuundwa serikali ya mseto. Katika suala hilo, kumezungumzwa na bado kunazungumzwa mengi. Hata hivyo Mwenzangu Othman Miraji alizungumza na Katibu wa uenezaji na itikadi wa CCM Bw John Chiligati ambaye kwanza alikaua na haya ya kueleza kuhusu matokeo ya kikao hicho cha Dodoma.

Tunarudi tena Afrika magharibi ambako rais Blaise Compaore wa Burkina Faso alitoa wito wa kuanza tena maandalizi ya uchaguzi

Blaise Compaore

Rais Blaise Compaore wa Burkina Faso

nchini Ivory Coast, baada ya ghafla rais Laurent Gbagbo kulivunja baraza la mawaziri na tume ya uchaguzi, tukio ambalo bila shaka huenda likachelewesha uchaguzi uliopangwa mwezi ujao wa Machi.

Rais Compaore alikuwa mpatanishi kati ya pande zinazohasimiana huko Ivory Coast ambazo zilifikia makubaliano 2007 hasa baina ya waasi wa kaskazini wanaolidhibiti bado eneo hilo pamoja na wapinzani wa kiraia upande mmoja na serikali iliokuweko wakati huo chini ya uongozi wa rais wa sasa Laurent Gabagbo.

Taifa hilo lenye utajiri wa zao la Cocoa na wakati mmoja likitajwa kama lulu ya Afrika lilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe 2002-2003 vikiligawa pansde mbili kaskazini na kusini.

Rais Campaore pia ametoa wito wa kuundwa haraka serikali mpya itakayozihusisha pande zote husika, huku akiwaomba waivory Coast kuwa watulivu na wastahamilivu.

Wakati hayo yakitokaea huko Ivory Coast jirani yake katika eneo hilo Guinea ilifungua ukurasa mpya kuelekea demokrasia, baada ya kuundwa serikali ya mpito. Serikali hiyo inaongozwa na Waziri mkuu wa kiraia Jean Marie Dore akiwa ni ya watu 39 mchanganyiko wa raia na wanajeshi. Miongoni mwa mawaziri wake hata hivyo ni wanajeshi wawili wanaohusishwa na mauaji ya septemba mwaka jana dhidi ya waandamanaji zaidi ya 150 wa upinzani waliokusanyika katika uwanja wa michezo mjini Conakry kudai demokrasia. Hao ni Kapteni Claude Pivi na Luteni Kanali Moussa Tiegboro.

Pivi pia anabakia kuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais wakati Toegboro pia mnaendelea na wadhifa wake wa kukiongoza kikosi cha kupambana na madawa ya kulevya na uhalifu.

Watatezi wa haki za binaadamu wamepinga kuteuliwa wanajeshi hao wawili wakisema ni fedheha.

Kiongozi wa taifa anaendelea kuwa Jenerali Sekouba Konate aliye kaimu wadhifa huo baada ya kupigwa risasi Kapteni Moussa Dadis Camara na mmoja wa walinzi wake ambaye hadi sasa hajulikani aliko katika jaribio la kumuuwa mwezi Desemba mwaka jana . Camara anaendelea na matibabu nchini Burkina faso baada ya kutibiwa hapo awali huko Morocco.

Katika eneo la maziwa makuu,

Wawakilishi wa serikali za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pamoja na wale wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, walikutana Kigali mapema wiki hii, kujadiliana jinsi ya kufikia makubaliano ambayo yatafungua ni kwa wakimbizi wa nchi hizo mbili kurejea makwao kwa hiari yao.

Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Rwanda, ambao wakimbilia eneo la mashariki mwa kongo, huku Rwanda nayo ikiwahifadhi maelfu pia ya wakimbizi wa Kongo waliyoko katika kambi ya Gihembe wilayani Gicumbi. Mwandishi wetu mjini Kigali Daniel Gakuba alitutumia ripoti.

Tunamalizia kusini mwa Afrika ambako Robert Mugabe wa Zimbabwe

Robert Mugabe November 2008

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

alitamka mnamo siku ya Jumatano kwamba yeye pamoja na washirika wake katika serikali ya mseto nchini humo akimaanisha chama cha upinzani MDC kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai na tawi lililojitenga MDC ya Athur Mutambara wamekubaliana kwamba vikwazo vinapaswa kuondolewa. Matamshi yake yalikuja siku moja baada ya Umoja wa ulaya kurefusha kwa miezi 12 mengine hatua yake ya kuwapiga marufuku masahibu kadhaa wa Mugabe kuingia katika nchi 27 wanachama wa Umoja huo, na kuzuwia mali za Mugabe na maafisa wake wapatao 100.

Pamoja na hayo akizungumzia uamuzi wa Umoja wa Ulaya , Rais Mugabe alisema hashangazwi akiongeza " Tunajua msimamo wao, hawataki mtu yeyote au nchi yoyote duniani kupiga hatua ya maana ya maendeleo. Uhusioano baina ya Zimbabwe na Umoja wa Ulaya umezorota kwa karibu miaka 10, ikitokana na machafuko yanayohusiana na uchaguzi na madai ya ukiukaji wa haki za binaadamu wa serikali ya Mugabe na chama chake cha Zanu-PF, ambayo mara nyingi hufungamanishwa na mpango wa mageuzi ya ardhi uliowalazimisha wazungu kutoa sehemu kubwa ya ardhi zao za kilimo kwa serikali iliodai kwamba ni kuwagawia waafrika wasio na ardhi. Lakini kumekuweko na malalamiko makali kwamba mashamba mengi yamechukuliwa na vigogo na wapambe wa rais Mugabe.

Mwandishi:Abdul-Rahman,Mohammed /Reuters/AFP/Correspondents

Mhariri: Miraji Othman

Sauti na Vidio Kuhusu Mada

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com