David Cameron atangaza kujiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.06.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

David Cameron atangaza kujiuzulu

Upande uliokuwa ukitaka utengano ulipata ushindi wa jumla ya asilimia 52, huku upande uliokuwa ukitaka Uingereza kusalia kwenye Umoja wa Ulaya ukipata asilimia 48. Washindi wa kura hiyo wasema matokeo ni uhuru wa nchi.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ametangaza kuwa atajiuzulu ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu. Hii ni baada ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya kupitia kura ya maamuzi iliyopigwa jana nchini humo.

Upande uliokuwa ukitaka utengano ulipata ushindi wa jumla ya asilimia 52, huku upande uliokuwa ukitaka Uingereza kusalia kwenye Umoja wa Ulaya ukipata asilimia 48.

Ni kufuatia matokeo hayo, ambapo waziri mkuu David Cameron ambaye alikuwa akiongoza kampeni ya kutaka Uingereza kusalia kwenye Umoja wa Ulaya, ametangaza kuwa hana budi kujiuzulu kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo ili kumpisha waziri mwengine mpya atakayeongoza Uingereza katika kukamilisha mchakato wa kujiondoa kwenye muungano huo, ambao sasa utasalia na wanachama 27.

Cameron anasema "Ninafikiria nchi inahitaji uongozi mpya. Sifikirii itakuwa sawa kwangu kujaribu kuwa nahodha kuongoza nchi kupiga hatua za mbele. Hakuna haja ya ratiba maalum. Nitaendelea kuhudumu katika wadhifa wangu kwa miezi mitatu ijayo. Waingereza wamefanya uamuzi unaopaswa kuheshimiwa na nitafanya kila juhudi kuisaidia japo nilikuwa upande mwengine"

Nigel Farage na wenzake wakisherehekea ushindi.

Nigel Farage na wenzake wakisherehekea ushindi.

Furaha kwa washindi

Nikel Farage ambaye ni mmoja wa viongozi waliokuwa wakiongoza utengano amesema uamuzi wa kura hiyo ni uhuru wa Uingereza na mwamko mpya wa jinsi Uingereza itakavyoendesha mambo yake. Anaongeza "Muungano wa Ulaya unaporomoka, Muungano wa Ulaya unakufa."

Farage ameendelea kusema "Ninayo matumaini tumeangusha tofali la kwanza, ninatumai hii ni hatua ya kwanza kuelekea kwa Umoja wa Ulaya ambapo mataifa yanayo mamlaka yao wenyewe. Sasa tunahitaji serikali ya utengano. Serikali itakayoanza kazi ya mijadala ya uhusiano kibiashara, itakayojali kuwa kuna makampuni mengi ya Ujerumani yanayounda magari na yanataka mikataba nasi. Sasa tuko huru kuanza mikataba yetu na mahusiano na mataifa mengine ya ulimwengu."

Hata hivyo matokeo hayo yameendelea kuigawa Uingereza jinsi tu kampeni za kura hiyo ziligawanya waingereza na hata Muungano wa Ulaya kwa Jumla. Scotland ambayo ni nchi ndani ya Uingereza ilipiga kura ya kutaka Uingereza kusalia ndani ya Muungano wa Ulaya, lakini ikazidiwa nguvu na matokeo kutoka maeneo mengine.

Mgwanyiko zaidi Uingereza

Hali inayokisiwa huenda Scotland ikajiona kama sehemu ya Muungano wa Ulaya, na ikizingatiwa kura yake ya kutaka kujitenga na Uingereza mwaka 2014 ilishindwa, huenda matokeo haya yakafufua juhudi za utengano wa Scotland kutoka Uingereza.

Hellen Waller mkazi wa Uingereza anasema "Ninafikiria ni wazo baya. Ninafikiria watu wamepiga kura kwa kufuata mioyo yao badala ya akili na ni ushindi mdogo na kweli ninafikiri uamuzi mkubwa kama huo unapaswa kuwa na ushindi mkubwa"

Kauli kama hiyo pia inatolewa na Mai Futita ambaye ni mgeni nchini Uingereza. "Ninafikiria inaenda kuwa taabu sana kwa wageni. Ninafikiri itakuwa ngumu kwa wasiokuwa raia wa muungano wa Ulaya kuja Uingereza kufanya kazi au kusoma labda ndivyo hali itakavyokuwa."

Miongoni mwa wanaopigiwa upatu kuwania wadhifa wa Waziri Mkuu ni aliyekuwa Meya wa London Boris Johnson na waziri wa haki Michael Gove ambao wamekuwa wakiongoza kampeni za utengano. Uingereza ndiyo nchi ya kwanza kujitenga na Muungano wa Ulaya.

Hali ambayo imezua msukosuko kiuchumi, kiuhusiano, kisiasa na njia mbalimbali huku athari ikitarajiwa itasambaa hadi mataifa mengine ambayo ni washirika wa Uingereza na Umoja wa Ulaya. Baada ya matokeo hayo, mchakato wa kisheria wa Uingereza kujiondoa rasmi kwenye Muungano wa Ulaya ndio sasa unafuata.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE/APE

Mhariri:

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com