Croatia yasonga mbele katika EURO 2008 | Michezo | DW | 13.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Croatia yasonga mbele katika EURO 2008

Ujerumani yabwagwa mara hii nchini Austria

Kutoka kushoto,wajerumani Michael Ballack, Per Mertesacker, Lukas Podolski na Philipp Lahm wakiondoka uwanjani baada ya kufungwa 2-1 na Croatia.

Kutoka kushoto,wajerumani Michael Ballack, Per Mertesacker, Lukas Podolski na Philipp Lahm wakiondoka uwanjani baada ya kufungwa 2-1 na Croatia.

Katika mashindano ya soka kutafuta bingwa wa Ulaya mwaka huu yanayoendelea nchini Uswisi na Austria, leo bingwa wa kombe la Dunia Italy inateremka uwanjani ,huku Ujerumani ikiwa imetolewa kijasho na Croatia katika mchezo wao uliofanyika jana.

Timu ya taifa ya Croatia, imekuwa timu ya pili kufuzu kwa awamu ijayo ya robo fainali katika mashindano ya mwaka huu ya kombe la Ulaya.

Timu ya kwanza ilikuwa Ureno.

Kufuzu kwa Croatia kulitokea baada ya kipenga cha mwisho kulia katika mechi yake dhidi ya Ujerumani,ikiwa juu na mabao mawili dhidi ya moja la Ujerumani ambayo imewahi kulitwa kombe hilo mara tatu.

Baada ya mechi hiyo ambayo ilikuwa inafuatiliwa vikali hapa Ujerumani,kocha wa timu ya Ujerumani,Joachim Löw,alikiri kuwa vijana wake hawakucheza vilivyo‚'Nadhani kila mchezaji anajua kuwa hakucheza kulingana na uwezo wake.Na hivyo mchezo wetu haukuvutia na hatukucheza kwa nguvu.Tulipocheza dhidi ya Poland tulicheza vizuri.Lakini leo mchezo kama huo hatukufanikiwa kuucheza,’amesema Löw

Ingawa matokeo hayo yamewavunja moyo wajerumani wengi ambao walikuwa wakifuatilia mchezo huo kupitia runinga katika sehemu mbalimbali,lakini baadhi walifurahi,akiwemo huyu raia wa Poland ambae ni mhudumu katika mgahawa mmoja hapa mjini Bonn akitoa sababu zake. Anasema kuwa kwa kuwa Ujerumani iliifunga timu yake anasikia raha kuona kuwa Ujerumani nayo inashindwa.

Bao la kufutia machozi la Ujerumani,lilifungwa na mshambuliaji wao Lukas Podolski kunako dakika ya 79 za mchezo .

Matokeo hayo yanaifanya Croatia kusonga mbele na pia kuongoza kundi hilo na pointi 6.

Ujerumani sasa inasubiri mechi yake dhidi ya mwenyeji Austria itakayochezwa jumatatu. Aidha itailazimu ishinde na pia kusubiri matokeo kati ya mechi nyingine katika kundi hilo ya siku hiyo kati ya Croatia dhidi ya Poland.

Wenyeji Austria waliponea chupuchupu kushindwa katika mechi yake dhidi ya Poland baada ya kwenda sare ya kufungana bao moja.

Bao la Austria lilikuja baadae katika dakika za majeruhi kupitia mkwaju wa penalti uliopachikwa wavuni na mchezaji Ivica Vastic. Nalo bao la Poland lilibandikwa kimyani na Roger Guerreiro kunako dakika ya 30 ya mchezo.

Kibarua cha timu hizo mbili,Poland na Austria,ni angalu mojawapo kupata ushindi ili kuweza kusonga mbele katika awamu ya robo fainali.Austria haijawahi kufika katika michuano ya mwisho ya mashindano hayo, na mara hii ilifuzu kushiriki moja kwa moja kutokana kuwa ni mwenyeji mwenza wa mashindano hayo.

Mwenyeji mwingine ni Uswisi ambayo tayari imeshapigwa kumbo na kutupwa nje ya mashindano hayo.

Na hayo yakiarifiwa leo Ijumaa jioni bingwa wa dunia Italy inakutana dhidi ya Romania katika patashika lingine ambalo linatabiriwa kuwa kali. Italy ililambishwa tatu bila jibu na Uholanzi.

Homa inaonekana inaikumba timu ya Italy kwani ikipoteza tena mechi ya leo Ijumaa katika kundi C linalochezea Zurich Uswisi mambo yake hayatakuwa mazuri.

Pia ikiwa Uholanzi nayo itaweza kuilaza Ufaransa,pia majaliwa ya timu ya akina Henri Thierry yatakuwa hayajulikani.

Ufaransa inaomba kuwa wachezaji wao wakutegemewa nahodha Patrick Vieira na mshambuliaji Thierry watateremka uwanjani baada ya kukosa uhondo wa mechi ya kwanza kutokana na majeraha.

 • Tarehe 13.06.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EJ7X
 • Tarehe 13.06.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EJ7X