1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Crimea kuomba rasmi kujiunga na Urusi

17 Machi 2014

Crimea leo itaomba rasmi kujiunga na Urusi, baada ya wakaazi wa eneo hilo jana (16.03.2014) kupiga kura ya maoni na kuamua kujitenga na Ukraine na kujiunga na Urusi.

https://p.dw.com/p/1BQln
Wakaazi wa Crimea wakishangilia baada ya matokeo kutangazwa
Wakaazi wa Crimea wakishangilia baada ya matokeo kutangazwaPicha: Reuters

Kura hiyo imefanyika wakati ambapo Ulaya inajiandaa kuiwekea Urusi vikwazo katika mzozo mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kati ya mataifa ya Mashariki na Magharibi, baada ya Vita Baridi.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi, asilimia 96.77 ya wapiga kura wamechagua kujiunga na Urusi na hivyo kuamua kujitenga na Ukraine, katika kura ya maoni iliyopigwa jana.

Bunge la Crimea kukutana leo

Bunge la Crimea litakutana leo kuomba rasmi kujiunga na Urusi, mchakato ambao unaweza ukachukua miezi kadhaa. Mkuu wa tume ya uchaguzi ya Crimea, Mikhail Malyshev, amesema idadi kubwa ya wapiga kura wameunga mkono hatua ya kujiunga na Urusi.

Kura hiyo ya maoni imekosolewa vikali kimataifa, na inaweza kusababisha ramani ya Ulaya kuchorwa upya, tangu mwaka 2008, ambapo Kosovo ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Serbia.

Rais Vladmir Putin akizungumza kwa simu na Rais Raback Obama
Rais Vladmir Putin akizungumza kwa simu na Rais Raback ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Marekani, Barack Obama alizungumza kwa njia ya simu na Rais Vladmir Putin wa Urusi na kumueleza kuwa kura hiyo imefanyika chini ya shinikizo la Urusi baada ya kuivamia kijeshi Crimea na kwamba kamwe haitatambuliwa na Marekani pamoja na jumuiya ya kimataifa.

Rais Obama ametishia kuchukua hatua zaidi kwa Urusi, baada ya wiki iliyopita kuweka vikwazo vya marufuku ya visa vinavyowalenga wale wanaodaiwa kutishia uhuru na mshikamano wa taifa la Ukraine. Aidha, Umoja wa Ulaya umesema kuwa kura hiyo ya maoni siyo halali na matokeo yake hayatatambuliwa.

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya kukutana leo

Wakati huo huo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana leo kujadili vikwazo vya kuiwekea Urusi, ikiwemo marufuku ya kupatiwa visa na kuzuia mali za viongozi wa nchi hiyo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine AshtonPicha: Reuters

Viongozi wa Umoja wa Ulaya, pia wametishia kuufuta mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi, uliopangwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu, iwapo Urusi haitoacha kujihusisha na mzozo wa Ukraine.

Mwishoni mwa wiki, Umoja wa Ulaya umefanya kazi ya kuorodhesha majina ya walengwa wa vikwazo hivyo.

Mmoja wa wanadiplomasia ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema orodha hiyo ndogo, lakini yenye umuhimu kisiasa, itapeleka ujumbe siyo tu kwa Crimea, bali pia kwa Urusi.

Waziri wa mpito wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andriy Deschytsya, atakuwepo leo mjini Brussels, lakini hatohudhuria mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya na badala yake anatarajiwa kukutana na Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,DPAE,AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba