1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19 yapoteza ajira za watu milioni 6 Marekani

Sylvia Mwehozi
2 Aprili 2020

Wafanyakazi milioni 6.6 nchini Marekani wamejiandikisha katika orodha ya posho ya wasio na ajira wiki iliyopita, ikiwa ni rekodi kubwa kuwahi kushuhudiwa, wakati virusi vya corona vikisababisha biashara nyingi kufungwa

https://p.dw.com/p/3aN3k
Deutschland Berlin - Frau mit Smartphone
Picha: picture-alliance/dpa/K. NIetfeld

Kiwango cha maombi ya mara ya kwanza ya posho ya wasio na ajira katika wiki ya mwisho wa mwezi Machi kilikuwa mara mbili ya kile kilichorekodiwa wiki moja kabla cha watu milioni 3.3 nchini Marekani. Kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya kazi ya Marekani, "karibu kila jimbo lilitoa sababu ya COVID-19", na kubainisha athari kubwa katika nyanja tofauti za kiuchumi hususan mahoteli, lakini pia viwanda na biashara ya rejareja.

Kwa upande wa Ujerumani waziri mwenye dhamana ya kusimamia uchumi Peter Altmaeir amesema uchumi wa taifa hilo huenda ukaporomoka zaidi mwaka huu ukilinganisha na kipindi cha mdororo wa uchumi wa mwaka 2008-2009.

EU Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Reuters/F. Lenoir

Altmaeir amesema uchumi wa Ujerumani ulikuwa katika hali nzuri katika kipindi cha miezi miwili ya mwanzo wa mwaka kabla ya taifa hilo kuchukua sehemu ya hatua za kufungia miji yake mnamo mwezi Machi, na akaongeza kwamba uchumi utaathirika zaidi mwezi huu wa nne na pengine unaweza kuanza kufufuka tena mwezi Mei. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen amesema bajeti ijayo ya muungano huo itakuwa "mpango wa ufufuaji uchumi" kwa ajili ya Ulaya. 

"Halmashauri itatoa mikopo kwa nchi wanachama wanaohitaji, kuimarisha mfumo wa muda mfupi wa kazi. Mifumo hii sasa ipo na imepangwa kutumika ndani ya Umoja wa Ulaya na itawanufaisha nchi wanachama wanaotaka kuitumia".

Nchini India waziri mkuu Narendra Modi amesema wataondoa hatua za wiki tatu za kuwazuwia raia, wakati maafisa wakijishughulisha zaidi kukabiliana na mripuko wa virusi hivyo katika mji ambao umetikiswa zaidi wa New Delhi. Hatua hizo ambazo zimesababisha uchumi wa taifa hilo la tatu kiuchumi barani Asia kusimama, zitafikia kikomo mnamo Aprili 14.

Symbolbild Coronavirus Homeschooling
Mtoto wa miaka mitano akiendelea kujifunza kutokea nyumbaniPicha: picture-alliance/empics/I. West

Modi amewaeleza mawaziri wake kuwa hata hivyo hatua hizo zimesaidia kupunguza maambukizi lakini hali bado si ya kuridhisha ulimwenguni na hivyo kunaweza kuwa na awamu ya pili ya wimbi la maambukizi. Huko Zambia, mtu mmoja amefariki kutokana na virusi vya corona, huku visa vya mambukizi vikiongezeka hadi 39. Kwa ujumla Afrika sasa imeorodhesha visa takribani 6000 vya COVID-19 na vifo zaidi ya 200.

Saudi Arabia yenyewe imetangaza marufuku katika miji yake miwili mitakatifu ya Macca na Madina katika hatua zake endelevu za kukabiliana na maradhi hayo. Marufuku hiyo ya saa 24 inaanza kutumika Alhamis hadi hapo itakapoondolewa.

Vyanzo: AFP/Reuters/DPA