1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19 ni mtihani mkubwa kwa Wakenya kujikimu kimaisha

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.19 Februari 2021

Wakenya 9 kati ya 10 wanasema hali yao ya uchumi itadorora zaidi iwapo ugonjwa wa COVID-19 utaendelea kuenea.

https://p.dw.com/p/3paXM
Mwanafunzi aliyegeukia ukahaba Nairobi wakati shule zilipofungwa
Mwanafunzi aliyegeukia ukahaba Nairobi wakati shule zilipofungwaPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture-alliance

Utafiti uliotolewa unaelezea namna mtazamo na tabia ya Wakenya ilivyobadilika, wengi wao wakijizatiti kuyakabili makali ya njaa, magonjwa na ukosefu wa usalama. Haya yanajiri wakati serikali inatangaza kusimamisha mpango wa ajira wa kazi kwa vijana.

Utafiti uliotolewa na Shirika la Twaweza la Afrika Mashariki unaeleza kuwa Wakenya sita kati ya 10 hawana uwezo na kupata lishe mara tatu kwa siku kutokana na athari za janga la ugonjwa wa COVID-19.

Soma pia:

Kenya yarefusha marufuku ya usiku wakati shule zikifunguliwa

Wahudumu wa maabara Kenya watishia kugoma

Ripoti ya matokeo ya utafiti huo iliyopewa jina, kujifunza kuishi na corona, inaelezea kwamba kuna ufahamu mzuri wa ugonjwa wa COVID-19 na juhudi za kujikinga zimeimarishwa kufuatia kampeini za wizara ya afya, ila kiasi kikubwa cha Wakenya wana wasiwasi wa familia zao kulala njaa, kukosa huduma njema ya afya mtu anapokuwa mgonjwa na usalama wa vyanzo vyao vya kujipatia ajira.

Utafiti umeonesha kuwa Wakenya sita kati ya 10 hawana uwezo na kupata lishe mara tatu kwa siku
Utafiti umeonesha kuwa Wakenya sita kati ya 10 hawana uwezo na kupata lishe mara tatu kwa sikuPicha: picture-alliance/ZumaPress/D. Sigwe

Je serikali imeshindwa kuwakinga wasiojiweza?

Aidha, tisa kati ya 10 wanasema hali yao ya uchumi itakuwa mbaya zaidi iwapo ugonjwa wa COVID-19 utaendelea kuenea. Hali hii inaaminika kuchangiwa na serikali kushindwa kuwakinga wasiojiweza dhidi ya makali ya virusi vya corona.

Mwaka uliopita serikali ya Kenya ilipunguza ada ya ushuru kwa bidhaa na mishahara ya wafanyikazi wa umma walio katika kiwango cha chini, lakini hatua hii ilikuwa kwa muda tu.

Wafanyibishara kwenye sekta za elimu, jua kali, afya, uchukuzi na utalii pamoja na hoteli walipata pigo kubwa wakati huu, utafiti huu ukieleza kwamba asilimia 62 ya Wakenya wanaitaka serikali itoe ruzuku kuwawezesha wafanyibiashara kuinuka tena.

Mpango wa serikali kwa vijana ‘Kazi mtaani' kumalizika Machi

Kinaya ni kwamba, hata mpango wa kuwainua vijana, uliopewa jina ‘Kazi mtaani' unafikia kikomo mwezi Machi mwaka huu baada ya serikali kusema haina fedha ya kuendelea kuufadhili. Msemaji wa serikali Cyrus Oguna amesema baada ya mpango huo kukamilika vijana wanafaa warejee kwenye kazi zao za awali ili serikali ipate ushuru.

Benki Kuu ya Kenya imetangaza kwamba imetoa shilingi bilioni tano kwa wizara ya fedha, kama malipo ya kipekee kuisadia serikali kuumudu mzigo uliosababishwa na makali ya janga la COVID-19.

Ili kukabiliana na wimbi la pili la virusi vya corona, Wakenya wamependekeza serikali iongeze juhudi katika kuidhinisha masharti yaliyowekwa na kuhakikisha uwepo wa huduma na vifaa vya afya.