Covid-19: Kenya yapiga marufuku mikutano ya kisiasa | Matukio ya Afrika | DW | 12.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Covid-19: Kenya yapiga marufuku mikutano ya kisiasa

Kenya imetimiza mwaka mmoja tangu kupata mgonjwa wa kwanza wa covid-19 kwa kuongeza muda wa kutotoka nje usiku kwa miezi miwili na kupiga marufuku mihadhara ya kisiasa kwa siku 30 ili kuzuwia virusi vya corona kusambaa.

Kwenye hotuba yake siku ya Ijumaa kuashiria mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza cha corona kutangazwa nchini Kenya, Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa hatoifunga nchi lakini ni lazima Wakenya wafuate maagizo ya afya yaliyopo.

Marufuku ya kutotoka nje usiku imeongezwa muda kwa miezi miwili ijayo kama njia moja ya kuepusha maambukizi mapya ya COVID-19.

Takwimu za masaa machache yaliyopita zinaonyesha kuwa maambukizo mapya yameongezeka kwa asilimia 13.2.

Kenia Coronavirus l Anti-Pandemie-Roboter namens Jasiri am Flughafen

Kenya imetumia mbinu mbalimbali kukabiliana na Covid-19, ikiwemo teknolojia ya kisasa kama roboti hii inayotumika katika uwanja wa ndege wa kimataifa ya Jomo Kenyatta kupima joto la abiria, utakasaji, kuwasilisha ujumbe wa kiafya na kukusanya data, iliyopewa jina la Jasiri.

Soma pia: COVID-19 Kenya: Muda wa kutotoka nje usiku wasogezwa siku 60

Tangu Rais Uhuru Kenyatta kulihutubia taifa mara ya mwisho tarehe 3 mwezi wa Januari mwaka huu, vifo vimeongezeka kutoka 1,685 hadi 1,899. Ili kuzuwia watu kukutana ovyo ovyo, mikutano ya kisiasa imepigwa marufu kwa muda wa siku 30 zijazo.

Wanasiasa wamekuwa wakiunadi mswada wa BBI kadhalika kuendeleza kampeni za chaguzi ndogo pasina kujali sheria za kuzuwia corona kusambaa kama vile kutosogeleana na kuosha mikono mara kwa mara.

Magavana waliomba mikutano ya kisiasa ipigwe marufuku kwa muda.

Wajibu wa kuwapokea wagonjwa wa COVID-19 unawaangukia viongozi wa kaunti ziliko hospitali za mikoani. Inasadikika kuwa wimbi la tatu la maambukizo ni kali zaidi na wadi za wagonjwa mahututi zimejaa.

Tazama vidio 02:23

Kenya na mapambano ya COVID-19

Raila Odinga aambukizwa Covid-19

Taarifa rasmi zinaeleza kuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM, Raila Odinga, ameambukizwa COVID-19 na anapata matibabu kwenye hospitali ya Nairobi.

Raila Odinga amekuwa akiyazuru maeneo kadhaa ya nchi ili kuuhamasisha umma kuhusu mswada wa BBI ambao unajadiliwa bungeni.

Soma pia: Tanzania yasema Rais Magufuli yuko buheri wa afya

Sehemu za ibada nazo pia zinashurutishwa kupunguza idadi ya waumini kuwa thuluthi moja pekee huku wanaohudhuria maziko na harusi wasipite watu 100. Wakati huo huo, maziko lazma yafanyike katika muda wa siku tatu baada ya mtu kufariki dunia.

Walimu kuchanjwa wiki ijayo

Yote hayo yakiendelea, chanjo ya corona iliyowasili nchini wiki moja iliyopita sasa imetua mikoani na wahudumu wa afya vile vile maafisa wa usalama wanaipokea.

Wiki ijayo, walimu walio na umri ulio zaidi ya miaka 50 wameratibiwa kuanza kuipokea chanjo hiyo ya AstraZeneca.

Weltspiegel 05.03.2021 | Corona | Kenia Nairobi | AstraZeneca-Impfstoff

Kenya imeanza pia kutoa chanjo ya Covid-19 kwa raia wake kuanzia mwezi Machi, 2021.

Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa kuchanjwa ni kwa hiari na kuwa chanjo hiyo ni salama ijapokuwa baadhi ya mataifa ya Ulaya yamesitisha matumizi yake kwa muda kwa madai ya madhara ya kiafya.

Awamu ya pili ya mpango huo wa chanjo ya corona utawashirikisha watu wazima na wale walio na magonjwa ya muda mrefu.