Corona: Nchi zazidisha vikwazo kudhibiti maambukizi | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Corona: Nchi zazidisha vikwazo kudhibiti maambukizi

Maambukizi ya virusi vya corona yanazidi kuongezeka kote duniani sawia na wale wanaokufa kutokana na virusi hivyo, jambo lililopelekea nchi kadhaa duniani kutangaza vikwazo vipya mwishoni mwa wiki.

Zimbabwe mwishoni mwa wiki ilitangaza kufunga nchi mara moja, nayo Gibralter ikachukua hatua sawa na hiyo, huku Ugiriki ikaongeza muda wa vikwazo vyake hadi Januari 10. Gavana wa mji wa Tokyo huko Japan ametaka hali ya dharura itangazwe huku Ufaransa ikitangaza marufuku ya kutotoka nje kuanzia saa mbili usiku hadi saa kumi na mbili alfajiri.

Kwengineko Ulaya, Ujerumani inatarajiwa kuongeza muda wake wa hatua za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona kupita Januari 10, muda uliokuwa umewekwa awali kutokana na ongezeko la maambukizi. Kulingana na wanasiasa nchini humu hospitali na wahudumu wa afya wanalemewa na mzigo wa wagonjwa. Kansela Angela Merkel na viongozi wa majimbo wanatarajiwa kukubaliana kuongeza vikwazo watakapokutana Jumanne. Bado haijawekwa wazi vikwazo hivyo vitaongezwa kwa muda gani.

Trump asema takwimu Marekani zimetiwa chumvi

Huko Marekani nchi ambayo imeathirika zaidi na virusi vya corona, hali inaendelea kuwa mbaya zaidi. Hapo Jumamosi watu 277,000 waliambukizwa virusi vya corona hiyo ikiwa ni rekodi ya maambukizi iliyowekwa kwa siku moja. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 350,000 wamefariki dunia nchini humo kutokana na virusi hivyo.

Großbritannien Oxford | Coronavirus | AstraZeneca Impfstoff

Brian Pinker apokea chanjo ya Oxford/Astrazeneca

Lakini Jumapili Rais Donald Trump alidai kwamba takwimu za maambukizi na vifo zimetiwa chumvi lakini maafisa wawili waandamizi wa afya walijitokeza na kupinga madai hayo ya Trump.

Katika masuala ya chanjo ya virusi hivyo Uingereza leo imechukua hatua nyengine kubwa katika mapambano ya Covid-19 kwa kuanza kutoa chanjo iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford na kampuni kubwa ya kutengeneza madawa ya Astrazeneca. Mtu wa kwanza kupokea chanjo hiyo ni Brian Pinker aliyepewa katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Oxford.

Afrika Kusini yatarajia chanjo kuanzia Februari

Kwengineko India ambayo ndiyo nchi ya pili iliyoathirika zaidi na virusi hivyo baada ya Marekani, Jumapili iliidhinisha kutumika kwa chanjo mbili ya kwanza ikiwa ya Oxford-Astrazeneca na ya pili ikiwa ni chanjo iliyotengenezwa nchini humo na kampuni ya kutengeneza madawa ya Bharat BioTech. Taasisi ya Serum nchini India ambayo ndiyo kubwa zaidi katika utengenezaji wa chanjo duniani imesema inatengeneza dozi milioni 50 hadi 60 kwa mwezi ya chanjo hiyo.

Coronavirus Indien Jammu | Corona-Test

Mwanamke apimwa virusi vya corona Jammu, India

Barani Afrika nako Afrika Kusini ambayo ndiyo nchi iliyoathirika vibaya katika bara hilo, inalenga kupata chanjo ya Covid 19 ifikiapo mwezi ujao wa Februari. Kulingana na waziri wa afya Zweli Mkhize, kwasasa bado wako katika mazungumzo na makampuni ya kutengeneza chanjo ingawa hakuna makubaliano yaliyoafikiwa.

Afrika Kusini inapambana na ongezeko la maambukizi kutokana na aina mpya ya kirusi kiitwacho 501V2. Nchi hiyo imeandikisha zaidi ya maambukizi milioni moja na vifo vimepindukia 29,000.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com