1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Covid-19: Marekani yarekodi maambukizi 67,000 ya siku moja

John Juma
16 Julai 2020

Marekani imeweka rekodi nyingine mpya wa maambukizi mengi ya corona. Kulingana na takwimu za chuo kikuu cha Johns Hopkins, watu 67,000 wamethibitishwa kuambukizwa kwa siku moja. 

https://p.dw.com/p/3fO7s
Coronavirus USA Miami Beach infizierte Person
Picha: Imago Images/Zuma/D. Santiago

Marekani ambayo ndiyo nchi inayoongoza ulimwenguni kote kwa idadi ya walioambukizwa virusi hivyo, imekuwa ikirekodi maambukizi ya juu tangu mwisho wa mwezi Juni, haswa kusini na magharibi mwa nchi hiyo.

Kwa siku 10 zilizopita, idadi ya watu wapya ambao wamekuwa wakiambukizwa nchini humo, wamekuwa kati ya 55,000 hadi 65,000 kila siku.

WHO: Maambukizi ya virusi vya corona yaongezeka ulimwenguni

Wakati huo huo, kuna kile kinachotizamwa kama mvutano kuhusu namna ambavyo serikali ya rais Donald Trump inavyolishughulikia janga hilo.

Mnamo Jumatano, mtaalamu na pia mkuu wa idara ya magonjwa ya kuambukiza nchini humo Daktari Antony Fauci, alisema haelewi juhudi za baadhi ya maafisa wa Ikulu ya White House kumdharau lakini anaamini hilo ni kosa kubwa.

Mvutano kuhusu corona Marekani

Kumekuwa na kile kinachotizamwa kuwa tofauti kati ya Antony Fauci (kushoto) na baadhi ya maafisa wa Iku ya White House kuhusiana na masuala ya kudhibiti janga la COVID-19.
Kumekuwa na kile kinachotizamwa kuwa tofauti kati ya Antony Fauci (kushoto) na baadhi ya maafisa wa Iku ya White House kuhusiana na masuala ya kudhibiti janga la COVID-19.Picha: Getty Images/Afp/M. Ngan

Kwenye mahojiano na jarida la habari la The Atlantic, Daktari Fauci amesema juhudi hizo za maafisa wa White House ni jambo lisilo la kawaida.

Mnamo siku ya Jumanne, Rais Donald Trump alimkosoa mshauri wake mkuu wa masuala ya biashara Peter Navarro, akisema hakupaswa kuchapisha maoni yake makali yaliyomkosoa Antony Fauci, ambaye ni mtaalamu mkuu wa serikali kuhusu masuala ya corona na ambaye pia ni maarufu.

Navarro aliandika kuwa japo Fauci ana uhusiano mzuri na umma, baadhi ya kauli zake ni makosa.

Wakati mwingine, kumeibuka mzozo kati ya Rais Trump na Fauci, huku Trump akitaka kufungua nchi ili watu warudi kazini. Vilevile amekuwa akitaka shule zifunguliwe kwa wanafunzi kuendelea mbele na masomo. Lakini Fauci amekuwa akishauri kuwa hatua hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari kuu, ili kuepusha kusambaa kwa virusi vya corona.

Kwa jumla zaidi ya watu milioni tatu wamethibitishwa kuambukizwa nchini Marekani na zaidi ya watu 137,000 wamefariki tangu janga hilo lilipoanza.

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro, angali augua COVID-19

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amesema amefanya vipimo vya pili na kugunduliwa kuwa angali ana virusi vya corona.
Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amesema amefanya vipimo vya pili na kugunduliwa kuwa angali ana virusi vya corona.Picha: picture-alliance/dpa/E. Peres

Kwingineko rais wa Brazil Jair Bolsonaro ameambukizwa tena virusi vya corona, lakini amesema kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa yuko salama.

Mnamo siku ya Jumanne, Rais Bolsonaro aliye na umri wa miaka 65, na ambaye pamoja na serikali yake wamekuwa wakipuuza makali ya ugonjwa wa COVID-19 kwa miezi kadhaa, alisema alifanya vipimo tena na kugunduliwa kuwa angali ana virusi hivyo.

Brazil imerekodi maambukizi milioni 2 ya COVID-19, hivyo kuwa taifa la pili baada ya Marekani miongoni mwa nchi ambazo zimeathiriwa zaidi.

Vile vile zaidi ya watu 75,000 wamefariki nchini humo kutokana na virusi hivyo vya ulimwenguni kote.

Wataalamu wanadhani kwamba huenda idadi ya maambukizi yako juu zaidi, katika taifa hilo lenye jumla ya watu milioni 210.

Awali Bolsonaro hakutaka kuvaa barakoa. Alihimiza uchumi wa taifa hilo kufunguliwa licha ya janga la corona, akihoji kuwa ugumu wa kiuchumi unaweza kusababisha vifo zaidi.

Mataifa mengi yamelazimika kusitisha mipango yao ya kuondoa vizuizi vya kuepusha virusi hivyo kusambaa zaidi.

Vyanzo: AFPE, DPAE,