1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP27: Mataifa makubwa yaunda muungano wa nishati ya upepo

Mohammed Khelef
9 Novemba 2022

Wakati mkutano wa kimataifa juu ya mabadiliko ya tabianchi, CPO27, ukiingia siku yake ya tatu nchini Misri, mataifa tisa makubwa ulimwenguni yamejiunga na umoja wa kuzalisha nishati kwa njia ya upepo wa bahari.

https://p.dw.com/p/4JFSi
UN- Weltklimakonferenz COP27 - Kanzler Olaf Scholz
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Uingereza, Ujerumani, Marekani na Japan ni miongoni mwa nchi zilizotangaza kujiunga na muungano wa kushajiisha uendelezaji wa nishati ya upepo wa mawimbi ya bahari, kwa jina la GOWA.

Muungano huo ulioasisiwa kwa lengo la kuondosha vikwazo vya kupata nishati, ulianzishwa awali na Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) Denmark na Baraza la Nishati ya Upepo Duniani. 

Mataifa mengine yaliyojiunga na muungano huo hapo siku ya Jumatatu (Novemba 8) ni Ubelgiji, Colombia, Ireland, Norway na Uholanzi.

Ägypten l COP27 Konferenzbereich im ägyptischen Ferienort Sharm el-Sheikh
Picha: Sayed Sheasha/REUTERS

IRENA na Shirika la Nishati Duniani (IEA) wanatabiri kwamba kufikia mwaka 2050, nishati itokanayo na upepo wa bahari itapindukia jigawati 2000 kutoka 60 za sasa, hatua ambayo itasaidia kuzuwia kupanda kwa joto kwa zaidi ya nyuzi 1.5 za kabla ya zama za viwanda.

Ulaya yategemea makubwa 

Mjumbe wa mabadiliko ya tabianchi wa Ujerumani, Jennifer Lee Morgan, ambaye nchi yake ni ya tatu kwa kuzalisha nishatihiyo duniani, alisema "kuna mipango ya kuongeza pakubwa utowaji wa nishati ya upepo wa mawimbi ya bahari."

"Bahari ya Kaskazini itageuka kuwa mtambo mkubwa kabisa na endelevu wa kuzalisha umeme na kuchukuwa nafasi ya gesi na mafuta kwa haraka." Alisema Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Tinne Van der Straeten.

Uingereza kutowa mikopo nafuu

Katika hatua nyengine, Uingereza imesema inapanga kutoa mikopo mipya kuzisaidia nchi ambazo zimeathirika zaidi kwa majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano wa kilele wa Tabianchi, COP27 waanza Misri

Wizara ya fedha ya nchi hiyo imesema kwenye taarifa yake ya leo kwamba mikopo hiyo itajumuisha kipengele kinachowaruhusu wakopeshwaji kuacha kulipa madeni yao endapo nchi zitakuwa zimekumbwa na majanga hayo.

Shirika la ukopeshaji wa nje wa Uingereza (UKEF) ndicho chombo kilichokabidhiwa jukumu la mikopo hiyo, ambayo itatolewa kwa mataifa yenye kipato cha chini na visiwa vidogo vidogo.

Wizara ya fedha ya Uingereza ilisema kwamba taarifa za kina juu ya mpango huo zitatolewa kwenye mkutano huu wa COP27.

"Nina fakhari kusema kwamba Wakala wa Ukopeshaji wa Nje wa Uingereza ndiyo wa mwanzo kabisa duniani kutoa mikopo ambayo itasitisha malipo ya huduma ya madeni kwa nchi zinazokumbwa na majanga ya tabianchi na ya kimaumbile." Alisema Naibu Waziri wa Fedha wa Uingereza, James Cartlidge.

Wasiwasi watanda Ulaya

Ägypten l COP27 Konferenzbereich im ägyptischen Ferienort Sharm el-Sheikh
Picha: Sayed Sheasha/REUTERS

Hayo yakijiri, Shirika la Mazingira barani Ulaya (EEA) lilisema kuwa mabadiliko ya tabianchi yamegeuka kitisho kikubwa kwa afya na mustakabali wa binaadamu, ukitaja kiwango kikubwa cha joto, mafuriko, na moto unaowaka misituni kugeuka kuwa uhalisia wa maisha ya sasa.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwenye siku ya tatu yamkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Tabianchi unaoendelea nchini Misri, shirika hilo lilisema kulikuwa na idadi kubwa ya vifo kwenye majira ya kiangazi ya mwaka huu barani Ulaya vilivyotokana na kuongezeka kwa joto.

"Idadi hii inaweza kuo ngezeka endapo hakutakuwa na hatua za uhakika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi." Lilisema shirika hilo.