1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo yasogeza mbele uchaguzi wa majimbo mawili

Admin.WagnerD26 Desemba 2018

Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imetangaza leo kuwa imeahirisha uchaguzi wa Disemba 30 kwenye maeneo kadhaa nchini humo hadi  mwezi Machi mwakani kutokana na mlipuko wa Ebola na mapigano.

https://p.dw.com/p/3Aea2
Demokratischen Republik Kongo | Wahlkommision |  Wahlautomat
Picha: DW/F. Quenum

Tume ya uchaguzi CENI imesema leo kuwa uchaguzi umesogezwa mbele kwenye miji ya mashariki ya Beni na Butembo na mji wa magharibi wa Yumbi lakini uamuzi huo hautaathiri uchaguzi wa rais uliopangwa Jumapili ijayo.

Upigaji kura katika uchaguzi unaopangwa kufanyika  disemba 30 tayari ulishaahirishwa kwa wiki moja baada ya tume kusema moto uliozuka kwenye ghala la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi mjini Kinshasa ulitatiza uwezekano wa zoezi hilo kuendelea.

Kulingana na tume hiyo ucheleweshaji huo wa uchaguzi kwenye maeneo hayo hautathiri ratiba ya uchaguzi wa  rais ambao unafanyika kwa pamoja na uchaguzi wa bunge na majimbo.

Kwa mujibu wa CENI Matokeo ya uchaguzi wa rais yatatangazwa Januari 15 na rais mteule ataapishwa Januari 18 mwaka 2019.

Hata hivyo tume hiyo haikutoa maelezo yoyote juu ya ni vipi matokeo ya kura ya urais yatajumuishwa  na yale ya majimbo ambayo hayatapiga kura Jumapili ijayo ambayo uchaguzi umepangwa miezi miwili baada ya rais mpya kuapishwa.

Maeneo ambayo hayatapiga kura ni ngome  ya upinzani

Demokratische Republik Kongo - Wahl
Picha: Getty Images/AFP/L. Tato

Jumla ya wapiga kura milioni 1.3 wataathiriwa na ucheleweshaji huo kutoka jumla ya wapiga kura milioni 44 walioandikishwa kupiga kura kwenye taifa hilo la Afrika ya kati.

Maeneo ambayo uchaguzi umeahairishwa yanatajwa kuwa ngome muhimu kwa wanasiasa wa upinzani nchini DRC.

Tume ya uchaguzi imesema uchelewashwaji huo unatokana na kuendelea kwa mlipuko wa homa ya ebola mjini Beni katika jimbo la Kivu kaskazini na kitisho cha ugaidi pamoja na mashumbilizi ya wanamgambo wenye silaha kwenye mji wa Yumbi.

Uchaguzi mkuu ambao mwanzoni ulipangwa kufanyika Disemba 23  na kisha kusogezwa mbele hadi disemba 30 umeshacheleweshwa hapo kabla kwa miaka miwili na rais Joseph Kabila jambo lililosababsha kuzuka maandamano ya umma na lawama kutoka jumuiya ya kimataifa.

Upinzani unaweza kukasirishwa na uamuzi huo?

Kollage von den vier Top-Kandidaten DR Kongo

Upinzani umeshaelezea wasiwasi wake kuwa uchaguzi huo hautakuwa huru na wa haki.

Mmoja wa wagombea urais wa upinzani Felix Tshisekedi, alisema wiki iliyopita kuwa ikiwa uchaguzi wa Disemba 30 utaahirishwa kwa mara nyingine, wafuasi wake wataingia barabarani na kumuondoa rais Kabila mamlakani.

Saa chache kabla ya tangazo la tume ya uchaguzi, mwanasiasa mwingine wa upinzani Martin Fayulu aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa maradhi ya ebola yanaweza kutumika kama kisingizio cha kuahirisha uchaguzi wa jumapili.

Wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulizitolea wito pande zote nchini Congo kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, amani na kuaminika ili kulinda utulivu na uthabiti wa taifa hilo.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP/DPA

Mhariri: Sekione Kitojo