1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo yapuuza wito wa mazungumzo na waasi wa M23

Saleh Mwanamilongo
1 Novemba 2022

Serikali ya Congo imesema uhusiano baina yake na Rwanda utategemea jinsi serikali ya Kigali itakavyositisha kile Kongo inachoelezea kuwa ni uungwaji mkono kwa waasi wa M23 na uingiliaji katika maswala ya ndani ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4IvwU
Felix Tshisekedi und Paul Kagame | Präsidenten DR Kongo und Ruanda
Picha: SIMON WOHLFAHRT/AFP/Getty Images

Waziri huyo amesema hatua ya Kongo kumfukuza balozi wa Rwanda na kumrejesha nyumbani mkuu wa ubalozi wake mjini Kigali inaelezewa kuwa jibu kwa vitendo vya Rwanda. Christophe Lutundula, Naibu Waziri Mkuu na mkuu wa Diplomasia ya Kongo amesema kufukuzwa kwa Balozi Vincent Karega kunabadili kila kitu katika uhusiano baina ya nchi mbili hizo.

''Ukweli ni kwamba hii leo, wakati tukiwa tayari kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo, hatuwezi kuzingatia kwamba mamlaka za Rwanda bado zinastahili imani ya Wakongo na kwamba maslahi yao yanawiana na yetu. Ninaamini kuwa katika uhusiano wowote uaminifu na maslahi ya pande zote ni jambo muhimu.'', alisema Lutundula.

Hata hivyo, Lutundula amesema bado kuna dirisha la mazungumzo baina ya Kongo na Rwanda  katika kurejesha mahusiano mazuri. Amesema kabla ya hatua hiyo Rwanda inatakiwa kusitisha uungwaji mkono wa aina yoyote ile kwa makundi ya waasi mashariki mwa Kongo. Kila mara Rwanda imekuwa ikikanusha kwa nguvu shutuma hizo.

Maandamano ya raia

Wakaazi wa mji wa Goma waandamana kuipinga Rwanda
Wakaazi wa mji wa Goma waandamana kuipinga RwandaPicha: Michael Lunanga/AFP

Jana, maelfu ya watu waliandamana mjini Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini wakiishutumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa eneo hilo. Hiyo ni baada ya waasi wa M23 kudhibiti vijiji kadhaa mwishoni mwa wiki iliopita. Serikali ya Kinshas inakosolewa kwa kushindwa kudhibiti usalama wa raia wake kwenye maeneo hayo ya Kivu na Ituri.

Mpatanishi wa Jumuiya ya nchi ya Afrika Mashariki, EAC, rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta amezitaka pande zote kusitisha uhasama na kuendeleza mazungumzo mjini Nairobi baadae wiki.

''Kuingizwa jeshini kwa waliokuwa waasi... hayo hayawezekani tena''

Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Congo, Christophe Lutundula amesema mazungumzo na kundi la M23 yanawezekana tu endapo waasi hao wataweka chini silaha na kuondoka kwenye maeneo yote wanayokalia.

''Ikiwa masharti hayo yote yanatekelezwa na kundi hilo la M23, na kwamba halipo tena kundi la kigaidi, tutatahmini. Lakini mazungumzo hayo hayawezi kuwa kwa misingi ya ugawanaji madaraka, kuingizwa jeshini kwa waliokuwa waasi... hayo hayawezekani tena.''

Kundi la wapiganaji wa M23 walianza tena mapigano mwishoni mwa mwaka jana baada ya kukaa kimya kwa miaka karibu kumi. Linaishutumu serikali Kinshasa kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ya kuwajumuisha wapiganaji wake katika jeshi.

Lutundula amesema Kongo bado inasubiri kikosi cha wanajeshi wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki katika kukabiliana na makundi ya wapiganaji kwenye mkoa wa Kivu.