1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CONAKRY : Wanane wauwawa katika machafuko mapya

11 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCTQ

Kumezuka maandamano ya upinzani katika miji ya Guinea hapo jana ambapo watu wanane wameuwawa wakati vyama vya wafanyakazi vikiapa kuendelea na mgomo wa kazi ulio na madhara kwa taifa baada ya Rais Lansana Conte kumtangaza rafiki yake wa zamani kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.

Wapizani wa Conte wamesema Eugene Camara mwanchama mwandamizi wa chama tawala alietangazwa kuwa waziri mkuu hapo Ijumaa yuko karibu mno na ukoo wa rais kuweza kuwa mtu wa kuaminika kuongoza serikali.

Waandamanaji wameweka vizuizi barabarani vilivyokuwa vikiwa moto na kujaribu kushambuliwa ofisi za serikali za mitaa pamoja na kupambana na polisi kuanzia mji mkuu wa Conakry hadi Nzerekore mji ulioko mbali kama kilomita 500 kusini mwa nchi hiyo.

Afisa mwandamizi wa serikali aliekataa kutajwa jina ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba wako kwenye hatari ya kutangaza hali ya hatari kwa sababu hali imegeuka moja kwa moja kuwa uasi dhidi ya serikali.

Vyama vya wafanyakazi ambavyo vinasema Conte hafai tena kutawala baada ya kuwepo madarakani kwa miaka 23 wamempa rais huyo hadi Jumatatu kumteuwa waziri mkuu mpya kama alivyokubali kwenye makubaliano waliofikia wiki mbili zilizopita kukomesha mgomo wa taifa wa siku 18 uliopelekea kuuwawa kwa watu 90.