1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton ajitwisha lawama za mashambulizi ya Benghazi

16 Oktoba 2012

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton amesema anawajibika kwa kasoro za kiusalama katika kukabiliana na mashambulizi kwenye ubalozi wa mjini Benghazi yaliyomuua balozi na raia wengine 3 wa Marekani.

https://p.dw.com/p/16QcA
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: Reuters

Kwa mujibu wa vituo viwili vya televisheni vya kimarekani, CNN na Fox News ambavyo vimefanya mahojiano na waziri Hillary Clinton, waziri huyo amesema kwamba anawajibika binafsi na kasoro katika kuhakikisha usalama kwenye ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, kwa sababu yeye ni kiongozi wa idara inayohusika na suala hilo. Bi Clinton ambaye yuko katika ziara nchini Peru, amesema isingekuwa rahisi kwa rais Obama au makamu wake kujua kila kitu kwa wakati ule.

''Rais na makamu wake bila shaka wasingeweza kufahamu kwa undani kila kitu kilichokuwa kikifanywa na wataalamu wa masuala ya usalama. Wataalamu hao ndio wanaotathmini kitisho kilichopo na kufanya uamuzi juu ya namna ya kukabiliana nacho.'' Alisema Bi Clinton.

Ubalozi wa Marekani mjini Benghazi ukiungua moto baaya ya kushambuliwa na waandamanaji
Ubalozi wa Marekani mjini Benghazi ukiungua moto baaya ya kushambuliwa na waandamanajiPicha: REUTERS

Obama aiepuka Shari

Kwa hatua hiyo ya kujitwika lawama kuhusu kasoro hizo, Bi Clinton amempunguzia mzigo rais Obama, ambaye baadaye leo atakabiliana kwa mara ya pili na mpinzani wake wa chama cha Republican kwenye uchaguzi wa Rais, Mitt Romney.

Mitt Romney na chama chake wamekuwa wakiyatumia mashambulizi ya Benghazi kuzishambulia sera za Obama kuhusu nchi za nje. Wamekuwa wakiandika kwa wino uliokolea namna utawala wa rais Obama unavyotoa maelezo yanayokinzana juu ya kilichotokea wakati wa mashambulizi hayo, ambayo yalimuuwa balozi wa Marekani nchini Libya Christopher Stevens na maafisa wengine watatu wa Marekani. Bi Clinton amesema utata huo ni kitu cha kawaida wakati wa kile alichokiita 'ukungu wa vita'.

Tangazo la kwanza la utawala wa Obama baada ya mashambulizi yale yaliyofanywa tarehe 11 mwezi uliopita, lilisema mashambulizi hayo yalisababishwa na ghasia zilizofuatia kutolewa kwa filamu inayomkashifu mtume Mohammad, na hayakuwa yamepangwa. Baadaye, rais Obama na maafisa wengine wamegeuza kauli na kusema kuwa yalikuwa mashambulizi ya kigaidi.

Waziri Hillary Clinton amesema katika mahojiano na kituo cha Televisheni cha CNN kwamba asingependelea mkasa huo utumiwe kama silaha ya kampeni ya uchaguzi, akiongeza kuwa kwa uzoefu wake, Wamarekani watakuwa imara wakisimama pamoja.

Rais Obama na mpinzani wake Mitt Romney watakwana tena katika mdahalo wa 2 usiku wa leo (16.10.2012)
Rais Obama na mpinzani wake Mitt Romney watakwana tena katika mdahalo wa 2 usiku wa leo (16.10.2012)Picha: Reuters

Romney aitumia Benghazi kama turufu

Mitt Romney amekuwa akifanya juhudi kuyatumia mauaji ya Benghazi kuzitia doa sera za nje za Obama, ambaye amesifiwa kwa kufanikisha kuuawa kwa kiongozi wa mtandao wa al-Qaida, Osama bin Laden, na kuwarudisha nyumbani wanajeshi wa Marekani kutoka katika vita vya Irak na Afghanistan, ambavyo haviungwi mkono na wamarekani wengi.

Mashambulizi ya wa-republican yaliongezwa makali baada ya mdahalo wa makamu wa rais wiki iliyopita, ambamo makamu wa rais Joe Biden alisema yeye na rais Obama hawakujua kama kulikuwa na maombi ya kuongezewa ulinzi kwa ubalozi wa Benghazi. Kauli yake ilipingana na maelezo ya maafisa wa wizara ya mambo ya nchi za nje, ambayo yalikuwa yametolewa siku mbili kabla.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir